Kaimu Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa ambaye ni kocha msaidizi wa Yanga, amekerwa na kitendo cha klabu za Yanga na
Azam kukataa kuwaachia wachezaji wao kwa ajili ya kujiunga na timu ya taifa
inayojiandaa na mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) dhidi ya
Nigeria.
Katika orodha
ya wachezaji 28 walioitwa kuingia kambini ni Yanga na Azam pekee ambazo
hazijaruhusu mchezaji yeyote kwa kile kilichohofiwa ni presha ya mchezo wa Ngao
ya Jamii utakaopigwa Agosti 22, mwaka huu kati ya klabu hizo.
Aidha, Mkwasa amesema
mbali na kwamba kukosekana kwa nyota hao kunaathiri programu zake, amepanga
kutumia mchezo wa Ngao ya Jamii kupima viwango vya nyota aliowaita, iwapo
hataridhishwa nao, atawapiga chini.
Katika hilo,
Mkwasa amelazimika kuita nyota wengine 10 kutokana na Yanga na Azam kugomea
kuachia wachezaji wao ambao tayari wapo kambini.
“Kwa namna moja
ama nyingine, zimewakatalia wachezaji kutokana na presha ya mchezo wao (Ngao ya
Jamii), hivyo nimeamua kuongeza wengine 10 ili kuwa na kikosi kipana ili
tusipate tabu wakati wa mchujo wa mwisho kuelekea Uturuki.
“Ni kweli kuna
athari kutokuwepo kwao maana kila kocha ana falsafa yake kiufundishaji,
tunaamini kama tungekuwa nao kikosini ingesaidia kujua ‘fitness’ yao na
kuendana na mfumo wangu, lakini ndiyo hivyo.
“Kwa upande
mwingine mchezo wa Ngao ya Jamii utatusaidia kuangalia viwango vya wachezaji
ambao wameshindwa kufika kambini kutokana na klabu zao kukataa, iwapo
itaonyesha kuwa viwango vyao vipo chini kulinganisha na hawa tulionao kambini,
basi tutaachana nao,” alisema Mkwasa.
Kikosi cha
Stars kinatarajia kuondoka nchini Agosti 23, siku moja baada ya mchezo wa Ngao
ya Jamii kuelekea Uturuki ambapo kitaweka kambi ya siku 10 kujiandaa na mchezo
dhidi ya Nigeria utakaopigwa Septemba 5, mwaka huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment