August 22, 2015


Na Saleh Ally
YANGA imefanya usajili mzuri kwa maana ya kuangalia zile nafasi zilizokuwa na upungufu msimu uliopita. Utaona kwenye safu ya ushambuliaji, pamoja na kuwaongeza washambuliaji wazalendo, ameongezwa Donald Ngoma kutoka Zimbabwe.


Kwa upande wa kiungo, pia Yanga ilionekana kuchelewa lakini baada ya mechi za kirafiki, benchi la ufundi chini ya Hans van Der Pluijm, likaamua kumsajili kiungo Thabani Kamusoko kutoka Zimbabwe ambaye anaonekana kutuliza mambo pale kwenye ‘moyo wa timu’.

Nyuma, yaani kwenye safu ya ulinzi, pia kulikuwa na tatizo. Pamoja na kuwa na mabeki wengine kama Rajab Zahir, Yanga ilihitaji beki mzoefu ili ikiwezekana kuwapa mapumziko nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na pacha wake, Kelvin Yondani.

Yanga imemsajili beki anayeonekana ni mzoefu, huyu ni Vincent Bossou raia wa Togo ambaye anajiunga na kikosi cha Yanga akitokea Goyang Hi FC ya Vietnam ambayo aliichezea msimu mmoja tu.


Simjui vizuri Bossou wala kazi yake, lakini niweke wazi kwamba napinga kabisa picha yake akikabana na Didier Drogba kuonekana kama vile kigezo cha ubora wake.

Hata Cannavaro na Yondani wamewahi kuwakaba au kupambana na Drogba, Kaka, Robinho na wengine kibao. Hivyo ubora wake hauwezi kupatikana kwenye picha mnato.

Kabla ya Goyang Hi FC, Bossou pia aliichezea An Giang ya Vietnam kwa msimu mmoja pia na usisahau alijiunga nayo akitokea TDC Bihn Durong.

TDC Bihn Durong alijiunga nayo kutoka Becamex Bihn Durong na timu hizi mbili alizichezea ndani ya mwaka mmoja. Yaani mwaka 2013 alicheza timu mbili.

Rekodi yake kisoka inaonyesha hivi, msimu wa 2011-12 alikuwaa akiichezea Navibank Sai Gon na msimu mmoja kabla, yaani 2010-11, alikuwa Marantha FC ya kwao Togo ambayo alikuwa amejiunga nayo kwa mara ya pili akitokea Etoile du Sahel.



Alikulia kisoka Marantha FC ambako alipata mafanikio makubwa, alipojiunga na Etoile du Sahel, ndani ya miezi minne tu, mkataba wake ukawa umevunjwa. Hakuna maelezo sahihi kwamba je, kuvunjwa kulitokana na kiwango chake kuwa duni au malipo? Maana wale Waarabu nao hawaaminiki.

Binafsi niwe mkweli, nina hofu sana na Bossou kwa kuwa rekodi hazimbebi kuonyesha kweli ni difenda bora ambaye anaweza kuisaidia Yanga kwa mambo mawili.
Rekodi zake zinaonyesha huenda si beki mwenye rekodi nzuri kiafya, kwa maana ya majeraha, ndiyo maana kila anapoichezea timu moja ndani ya kipindi kifupi, anauzwa.

Pia inawezekana kiwango chake si kizuri au difenda huyo amekuwa msumbufu. Niseme hivi, inawezekana ana tatizo la nidhamu, ndiyo maana hadumu katika klabu moja kwa muda mrefu.

Ukiangalia rekodi inaonyesha hivi; ndani ya miaka 10, Bossou amezichezea timu nane, hii ni kuanzia 2006 hadi 2015. Na mara mbili, amezichezea timu mbili katika msimu mmoja.

Inawezekana tungetumia mwaka, basi atakapoichezea Yanga msimu huu katika ligi, atakuwa ameingia kwenye rekodi ya kucheza katika timu mbili pia mwaka 2015. Kwani tayari alishaichezea Goyang Hi FC. Maana yake atakuwa kacheza timu sita katika miaka mitatu na timu 9 katika miaka 10.

Bado inawezekana hili likawa halikushtui wewe hata kidogo, lakini mimi nimeona kuna jambo linakuja ambalo tukubali lazima haya mawili yatatokea.

Yanga inaweza kufaidika kwa kuwa Bossou atahadithiwa kuwa Saleh Ally ameishatibua mambo kwa kukuwekea hofu, basi jamaa atajituma vilivyo kumziba mdomo ili ashindwe kusema tena.

Pili; kuna uwezekano mkubwa, kama alivyofanya katika timu nyingine, Bossou ataondoka mapema Yanga, ingawa hatujui sasa ni kwa utukutu au kuwa na hasira kama atagoma kutokana na chochote.

Yote yanawezekana, lakini rekodi bado zinamuacha Bossou ‘mtupu’, hazimbebi! Naweza kusema, Yanga wanaweza kuwa wanajua zaidi ubora wake huenda kutokana na ‘clip’ za video au vinginevyo lakini ninaamini, kuna jambo linakuja, tuombe liwe la kheri.




2 COMMENTS:

  1. Kwanza hakuna mtu wa kwenda kumwambia mtogo eti wewe unamponda, hiyo ni defensive mechanism kwamba yasipotokea unayotaka basi ionekane kwamba alikusikia!! Pili ubora wake mbali na club ni kwenye timu ya taifa, ni mchezaji wa timu ya taifa hafi leo!! Kama amekuja hapa kwa kheri basi inamaana alikotoka ni salama cha muhimu ni mkataba gani wameingia

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic