Na Saleh Ally
MECHI ya pili kwa kila timu inaonekana wazi
Ligi Kuu Bara imeanza kupamba moto na hakika utamu wake unaanza kuonekana.
Kuna timu zimeshinda mechi zote mbili, hasa
vigogo na wakongwe kama Yanga, Simba, Mtibwa Sugar na Azam FC, lakini kuna zile
ambazo mambo yameenda vibaya na kupoteza mechi zote mbili.
Kupoteza zote mbili ni kutopata pointi hata
moja, lakini wapo ambao angalau wameambulia kutoka sare moja au sare na
ushindi. Ndiyo ligi imeanza na kila upande unaangalia suala la biashara
asubuhi.
Kama timu itajichanga katika kipindi hiki na
kufanya vizuri, ina nafasi ya kusonga na kujiweka katika nafasi nzuri ya
ubingwa tena mapema.
Suala ya kuona ni mapema sana, mambo
hayawezekani au lazima kusubiri hadi baadaye ndiyo kupotea huko, maana wapo
wanaozichanga pointi kipindi hiki, tena taratibu tu.
Wakati ligi inaanza kupamba moto, ya
kuzungumzia hayakosekani. Leo nalenga suala la ulinzi kwa wachezaji uwanjani na
hasa ukiangalia katika mechi chache tu za Ligi Kuu Bara.
Inaonekana kuna baadhi ya wachezaji hawana
malengo au wana malengo na wanaposhindwa kuyatimiza, huenda wanataka kuharibu
malengo ya wengine.
Rafu, ubabe wa kijinga, kucheza kwa kulenga
kuumiza, hakika haiwezi kuwa ni lengo la kufanikisha mambo kimichezo. Kuumiza
mwili si jambo sahihi hata kidogo.
Ulimuona Kocha Hans van der Pluijm wa Yanga
akimlalamikia mwamuzi kuhusiana na wachezaji wa Prisons ya Mbeya, kwamba
hawakuwa na mchezo wa kiungwana na walilenga kabisa kuwaumiza wachezaji wake.
Kocha wa Simba, Dylan Kerr alionyesha
kuchukizwa na mchezo wa wachezaji wa Mgambo, si kwamba walikuwa ni fiti sana,
lakini faulo hazikuwa za kimichezo.
Najua walengwa wakisoma hapa, watalalama
kwamba kwa kuwa Simba au Yanga wamefanyiwa ndiyo imesemwa. Ukweli ni hivi, awe
mchezaji wa timu yoyote anapaswa kujua soka la kiungwana ndiyo bora na lenye
mafanikio.
Kuumia kuna bahati mbaya, lakini si sahihi
kumuumiza mchezaji mwingine kwa makusudi, kwani hata uliyefanya kosa utabaki na
kitu moyoni ambacho kitakutafuna kwa ndani, hasa kama ni mstaarabu na unajali.
Tena kila mchezaji anapaswa kujua, kama yeye
kwake soka ni kazi, pia kwa mwingine ni kazi. Kwamba kama mwingine anaumia na
atakosa mengi na familia yake itaathirika, basi ajaribu kujifikiria ikitokea
kwake itakuwaje.
Uungwana ni kuangalia soka si vita, si
sehemu ya kuumizana, si sehemu ya kukwamishana, si sehemu ya kuzuia ndoto za
wengine. Hivyo ni jambo jema kuangalia soka la kiungwana.
Kama wachezaji wanaingia uwanjani wakiwa
wamepania kuwazuia wachezaji nyota au kutoka timu maarufu, basi washindane nao
kwa maana ya ushindani wa kisoka.
Beki Luke Shaw wa Manchester United
amevunjika mguu katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya walipokuwa wakipambana
dhidi ya PSV ya Uholanzi. Wakati anaumia, faulo ilionekana ni ya kimpira, hadi
sasa hakuna kulaumu na inaonekana ilikuwa bahati mbaya.
Jiulize aliyemuumiza angekuwa amefanya
makusudi, sasa angekuwa anajisikiaje? Ndiyo maana ninasisitiza lazima kuwe na
uungwana kwani soka ni mchezo unaohusisha wanadamu ambao wameumbwa na uungwana
ndani yake.
Kuumiza hakuwezi kuwa sehemu ya mafanikio,
kucheza kwa kutaka kukwamisha wengine hakuwezi kuwa chachu ya mafanikio tena
hata kidogo.
Ndiyo maana nasisitiza kwa wachezaji
kubadilika, lakini naisisitiza TFF kulisisitiza hili kwa waamuzi kwamba lazima
kuwe na ulinzi kwa wale wanaotaka kuumiza kwa makusudi, wapewe adhabu kali.
Wakati mwingine, binadamu asiyejielewa, ni rahisi
sana kubadilika na kufanya mambo vizuri kama akikumbana na dhabu. Hivyo, hili
lipewe kipaumbele ili tushuhudie soka likipambana kukua na si kukuza Kung Fu au
mieleka ndani ya soka.
0 COMMENTS:
Post a Comment