Na Saleh Ally
Umemsikia Msemaji wa
Yanga, Jerry Muro akizungumzia maandalizi ya kikosi cha Yanga kwa ajili ya
msimu mpya?
Kama haukumsikia, mimi
nilisikia akihojiwa na moja ya redio moja katika kipindi chake cha michezo.
Muro alikuwa akielezea namna Yanga ilivyo fiti.
Alikuwa akisisitiza
kwamba Yanga iko tayari kwa ajili ya mchezo wa Coastal Union ambao utakuwa ni
wa kufungua Ligi Kuu Bara kwao na kampeni yao mpya kwa ajili ya kuanza kuutetea
ubingwa wao.
Muro alijigamba,
nafikiri ni jambo zuri. Muro alitoa tambo akiwadhihaki Simba kwamba si wa
kimataifa, ambalo si jambo baya kwa kuwa hao ni watani.
Lakini Muro,
alichemsha baada ya kuingiza tambo zake katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa
Stars, jambo ambalo lilinivuta kuandika makala haya.
Wakati akijigamba,
Muro alisema Yanga ni ya kimataifa na kulidhibitisha hilo ni ule ukuta wa Taifa
Stars ambao kwa asilimia 90 uliundwa na wachezaji kutoka Yanga.
Aliwataja kipa Ally
Mustapha ‘Barthez’, beki wa kushoto Haji Mwinyi, beki nne Kelvin Yondani na
kitasa Nadir Haroub ‘Cannavaro’, wote wametokea Yanga.
Muro alisema wachezaji
wote hao, wanatokea Yanga na ndiyo maana Wanigeria walishindwa kufunga bao hata
moja na hiyo inaonyesha kiasi gani Yanga ni ya kimataifa.
Tambo kwa Yanga na
Simba, sawa kabisa kama ambavyo nimeanza kueleza. Lakini Muro amesahau
Watanzania wanaipigania kwa pamoja Taifa Stars kuhakikisha wanaiunga mkono
kweli?
Amesahau kwamba
Watanzania kwa asilimia kubwa wameanza kurejesha umoja, wameanza kuungana na
leongo ni kuifanya Taifa Stars bora na moja kwa ajili ya Watanzania.
Sijui kama Muro
anakumbuka kwamba kati ya vitu vilivyoua uzalendo katika kikosi cha Stars ni
watu kuendekeza Usimba na Uyanga.
Amesahau kwamba Usimba
na Uyanga ndiyo ulichangania mapenzi ya Stars kugawanyika. Ikawa hivi, kipindi
kikosi hicho kikiwa na Simba wengi, kinashangiliwa sana na Wanamsimbazi na
kubezwa na Wanajangwani na kikiwa na wachezaji wengi wa Yanga, basi Simba
hawakitaki huku yanga wakikiunga mkono kwa nguvu sana.
Sasa hayo yameanza
kufutika, wachezaji wengi wa kikosi hicho wanatokea Yanga na Azam FC. Simba
hawana wachezaji wengi lakini Wanasimba wanakiunga mkono kwa nguvu.
Huenda wako ambao
hawafurahii, lakini lazima tukubali Taifa Stars haiwezi kuwa timu ya ‘kubalansi’.
Vema kuangalia uwezo wa wachezaji na kujali kikosi ‘kitapafom’ vipi na kuleta
matokeo mazuri.
Sasa wakati wengine
wanaona umuhimu wa utaifa, kiongozi ambaye amepewa dhamana ya kuzungumza kwa
ajili ya klabu kongwe kabisa, anamwaga maneno kama hayo ya kuysambaratisha
umoja.
Muro, aisee Muro,
inabidi ubadilike kwa kuongeza umakini katika kauli zako. Lazima ujue wakati
husika wa kusema jambo fulani. Huenda uliangalia utani wenu zaidi na Simba,
lakini haukujua kauli yako itageuka kuwa sumu kwa taifa.
Tukianza mgawanyino
kwa sasa, maneno kama hayo, mwisho yataamsha hisia na watu watarudi hadi
kuhoji, vipi Mkwasa ni kocha wa Yanga, mbona hakuna kocha wa Simba, au lazima
na Matola aitwe.
Hivyo ni vizuri sana
kuliangalia hilo au kuangalia nini cha kuzungumza kulingana na wakati mwafaka. Kwani
hata kama ungesema Yanga ina safu bora ya ulinzi, ukawataja majina wachezaji
bila ya ksuema walifanya nini wakiwa Taifa Stars, ingekusaidia kujenga hoja
yako vizuri bila kusababisha mifarakano. Huenda ulipotea, sasa rudi kwenye reli
na kazima ujitambue, pia utambue kwamba unapozungumza inakuwa ni kwa niaba ya
Yanga na si niaba ya Muro.
0 COMMENTS:
Post a Comment