Na Saleh Ally
HIKI ndiyo kile kipindi cha siasa, wanasiasa wanajaribu kuzungumza
lolote wakiwa na nia ya kupata ‘kiki’.
Hata unieleze vipi, hauwezi kunitosheleza kuamini kwamba kweli wanasiasa
wanazungumza mambo kutoka mioyoni mwao wakiwa na lengo la kuwakomboa
Watanzania.
Wapo wenye nia hiyo tena ni wachache sana, lakini wengi ni wale ambao
wanataka kufanikiwa wanachokitaka na wengi ni nafasi za uongozi.
Siipendi siasa, imejaza watu wengi waongo na wabinafsi, watu
wanaotudanganya wananchi kila kukicha na mapenzi yao kwetu ya mayai mabichi,
wakati yoyote yanavunjika na kukuchafua.
Kati ya wanasiasa ambao ninawakubali ni Zitto Zuberi Kabwe, sitaki
kusema ni mkweli kuliko wote lakini angalau anaweza kuuridhisha moyo wangu
namna ambavyo amekuwa akipambana.
Mwanasiasa kijana aliyeipa sifa kubwa Chadema, wakamuona hafai. Safari
hii ameingia ACT, yaani kaanzisha chama chake na taratibu kinakwenda, hongera
kwake.
Lakini siku chache zilizopita, Zitto ‘alirudi’ nyumbani, kule ambako
wanasiasa wanakotokea. Sehemu ambayo wanajiangalia au kudanganya. Sehemu ambayo
wanataka kuonyesha ni wazuri sana kwa wananchi bila kujali wengine wataumia
vipi.
Akiwa anahutubia huko Mbagala, aliagiza eti TFF iache mashabiki waingie
bure katika mechi ya kuwania kucheza Afcon wakati Taifa Stars itakapokuwa
inapambana na Nigeria pale kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Waliokuwa kwenye mkutano ule, wakamshangilia kwa nguvu kwa kuwa vyovyote
vile, mashabiki watafurahia kuingia bure. Hilo halina ubishi maana mchezo wa
soka ni burudani ya wengi.
Mashabiki sawa wanashangilia, huenda wako walimuona muungwana sana.
Lakini hakika ukitafakari utaona ndiyo ujanja wa kisiasa kutaka kuitumia tu
michezo ili kujifaidisha na huo ndiyo ule ubinafsi ninaousema.
Zitto angekuwa amepata nafasi ya kuwa Katibu Mkuu wa Fat miaka 10
iliyopita asingefanya hivyo. Nilisimama sehemu ya waliompigia debe Zitto
alipowania ukatibu mkuu wa Fat, miaka hiyo zaidi ya 10 iliyopita.
Zitto alishindwa na Michael Richard Wambura. Tena kwenye uchaguzi huo
hakuwa na nafasi hata kidogo kwa kuwa waliokuwa wakichuana ni Wambura na
aliyekuwa katibu wakati huo Ismail Aden Rage ambaye aliangukia pua.
Nilikuwa kwenye timu ya Zitto kwa kuwa niliridhishwa na maneno mazuri
aliyoyatoa. Aliyoyapanga na kunuia kuyatekeleza, tatizo hakuwa hata na fedha ya
kampeni, ushabiki ulitawala na mazoezi yalimzidi nguvu, akashindwa na mimi
nikadondoka.
Sijakutana siku nyingi sana na Zitto, lakini baada ya kauli yake hiyo nilikuwa
najaribu kutafakari kama kweli angeshinda siku hiyo, leo akaendelea kubaki
kwenye mpira. Je, angekuwa tayari kuachia watu wote waingie Taifa Jumamosi,
bure! Naamini isingekuwa hivyo na huenda angekasirishwa sana na kauli ya
mwanasiasa kama aliyoitoa yeye, kuwa watu waingie bure.
Vipi Zitto hakusema ACT angalau inalipia hata watu wapatao 2,000 tu na
kushauri waliobaki walipiwe na vyama vingine au makampuni fulani.
Bado angeweza kuyashawishi makampuni, wafanyabiashara maarufu au vinginevyo kuwanunulia tiketi Watanzania wengi wapenda soka ukiwa ni mchango wake wa kuongeza nguvu kwa kikosi cha Stars, lakini siyo hicho alichokisema.
Zitto anajua kuwa soka ni gharama, vijana wameandaliwa kwa mamilioni ya
fedha ikiwemo kuwasafirisha Uturuki kuweka kambi. Mrisho Ngassa, Mbwana Samatta
na Thomas Ulimwengu wanatumiwa tiketi kwenda na kurudi katika timu zao.
Wanahudhumiwa wanapokuwa jijini Dar es Salaam na Stars inakaa kambini
tokea Uturuki hadi hapa nyumbani. Je, ni kweli yote haya Zitto hayajui? Alifikiri
kuisaidia TFF angalau kidogo kabla ya kutoa kauli hiyo inayolenga kumuonyesha
yeye na ACT wanajali wananchi lakini si TFF?
Je, mwananchi anakubali kwenda uwanjani bure huku akijua akifanya hivyo
atawaumiza hata vijana wanaopambana na Nigeria siku hiyo?
Kwangu naona Zitto hakuwa mzalendo, amekuwa mbinafsi, ametaka kuivika
TFF ubaya, ametaka aonekane ana huruma sana kuliko wengine wote, jambo ambalo
si sawa hata kidogo.
Wengi sana wangehofia kumweleza Zitto ukweli, huenda wataingia na
kuuvaaa ubaya ambao kama TFF watatoa kauli katika hilo, watauvaa. Wala sina
hofu, namsisitiza Zitto kukumbuka yeye ni mwanamichezo basi anapaswa kuwa
mkweli na anayewaonea huruma wanaoisaidia michezo kuliko kuangalia anapata nini
kwenye siasa kwa kusema tu ilimradi.
Kweli wako ambao hawawezi kutafakari na wataliona jambo hilo ni sahihi,
lakini wako wenye uwezo wa kung’amua kwamba Zitto alifanya siasa lahisi
kuwaumiza wanaoihudumia timu ya taifa, jambo ambalo si sawa hata kidogo na
itakuwa vizuri hii ikiwa ni mara ya mwisho kutumbukia huko kwa lengo la
kujiongezea anachotaka!
Wanasiasa ni shida na ni wabinafsi!! Na ndio maana wanatumia muda mwingi kuchafuana na kutuchanganya wananchi. Zitto ni mfano mzuri wa akina Slaa, Lipumba nk. It is time wananchi tuwe na upeo wa kuchambua kujua wanatuongopea!! Sema na nyie waandishi hamtusaidii kuchambua badala yake mnakuwa speaker tu!!
ReplyDelete