September 23, 2015

BOSSOU (KUSHOTO)
Na Saleh Ally
YANGA ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na watani Simba ndiyo waliolialia sana tu kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), wachezaji wa kigeni waongezwe.


Azam FC walikuwemo pia, walikuwa katika kundi la Yanga kwamba wao wanashiriki michuano ya kimataifa.

Kwa kuwa timu hizo ndiyo kubwa na zilikuwa zinalialia, TFF na TPLB hawakuwa na ujanja. Wakaonekana kuzidiwa nguvu, mwisho wakaongeza idadi hiyo.

Jaribu kufanya ingekuwa hivi, TFF na TPLB wangesimamia kwenye ishu ya kubaki na wachezaji watano. Yanga, Simba na Azam FC wangelalama sana, tena kwa kiasi kikubwa.

Lakini wameshinda, wameruhusiwa kusajili kwa idadi wanayoona wao ni sahihi. Lazima maneno yangekuwa mengi na ingeonekana kama wamekwamishwa.
 
COUTINHO AKIWA BENCHI
Huenda kingekuwa kisingizio kikubwa kama timu hizo zingetolewa mapema katika michuano ya kimataifa, jambo ambalo si geni hata kidogo.

Hata Simba nao wangelalama kwamba wamekwama kufanya vizuri kama walivyotaka kwa kuwa TFF imegoma kuongeza wachezaji wawili zaidi angalau wafike saba. Mwisho TFF imekubali kuwaongeza, lakini timu hizo na hasa wakongwe Yanga na Simba, wanaonyesha hawakuwa wamejindaa.

Yanga na Simba hawakuwa wamejiandaa kwa kuwa pamoja na kuongezeka kwa ruhusa ya kusajili wachezaji wawili zaidi. Usajili wao unabaki uleule wa wachezaji watano.

Simba kwamba hawanasajili wachezaji saba, wamefanya hivyo lakini hadi sasa inaonekana wawili wanabaki kuwa hawana faida hata kidogo. Kimsingi, baada ya mechi tatu, wachezaji angalau watatu hadi watano wa kigeni kwa viko vya Yanga na Simba ndiyo wanaoonekana kuwa wenye msaada.

Wawili hadi watatu wanaonekana wako hapa nchini kujifunza, jambo ambazo huenda kikawa kichekesho kipya kwa ajili ya kuwafurahisha wapenda soka na si kwa ajili ya manufaa ya vikosi hivyo kwa maana ya ushindi.


Kutokana na ruhusa ya TFF na TPLB, Simba ilisajili jumla ya wachezaji saba ambao ni
Justuce Majabvi (Zimbabwe), Hamisi Kiiza, Simon Sserunkuma, Juuko Murshid (wote Uganda), Pape Nd’aw (Senagal), Emiry Nimubona (Burundi) na Vicent Agbani (Ivory Coast).

Kwa upande wa Yanga wana Andrey Coutinho (Brazil), Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima (wote Zimbabwe), Thabani Kamusoko na Donald Ngoma (wote Zimbabwe), Amissi Tambwe (Burundi) na Vicent Bossou kutoka Togo.

Usajili wa kila upande ulijaa mbwembwe na majigambo, kwamba waliosajiliwa ni wachezaji wenye msaada mkubwa na hilo ndilo lengo.

Simba na Yanga, kila moja hadi sasa imeshuka dimbani mara tatu, zote zimeshinda mechi zote na wageni wameonyesha mchango mkubwa.

Lakini inaonekana kuna wageni wategezi, au hawana msaada na hawatakuwa mfano wowote kwa wazawa zaidi ya kuwaumiza kwa kuwa wako wanaonekana wana uwezo sawa au chini ya wazawa na hawakustahili kusajili.

Haiwezekani wakasajiliwa kama wachezaji wa kulipwa, wanaopata mishahara na huduma bora zaidi ya wazawa halafu wanauza sura tu kwenye mabenchi ya timu hizo, hii si sawa.

Asitokee Yanga au Simba, akasema huu si wakati mwafaka wa kulizungumza hilo. Wakati wote tunataka kuweka mambo wazi, bila ya upendeleo na Yanga na Simba, hazipaswi kuwa na watalii.

Yule beki, Bossou, kasajiliwa kuja kukaa benchi. Yaani hana uwezo zaidi ya Kelvin Yondani na Nadir Haroub Cannavaro, maana mechi tatu sasa hajacheza! Vipi alipwe mshahara mzuri, nyumba na posho juu halafu aonekane pale benchi ‘akiuza sura’.

Coutinho ni Mbrazil, anaozea benchi! Kocha hakujua kama hamhitaji kipindi hiki, kwa nini asingemuacha na nafasi ya kuozea benchi ikapungua na pia Yanga wakapunguza gharama na pia ikapatikana nafasi ya mzawa mmoja!

Angalia Simba, wana kipa wa kimataifa ambaye anawekwa benchi na Peter Manyika, kipa kinda kabisa. Huyu atakuja lini na vipi kashindwa kuwa namba moja.

Hali kadhalika, ‘tall’ Nd’aw inakuwaje yuko benchi na wazawa wanaonyesha kuwa na uwezo kuliko yeye. Hata alipoingizwa uwanjani, alionekana kama ‘mkaguzi’ wa wenzake!

Hata kwa utetezi gani, Yanga na Simba zinapaswa kuwa makini na zenye hesabu. Sidhani kama ni sahihi kusajili profesheno halafu eti anakuja kupata uwezo wa kucheza soka hapa.

Akija anatakiwa kucheza, si kuozea benchi akibeba mamilioni. Kama kweli wana uwezo umejificha, basi wapeni salamu na muwaambie waonyeshe kiwango na wakiwa hawawezi, vizuri waachie wazawa nafasi zao ili waendelee kupambana. Profesheno, aonyeshe kazi safi, si kuja hapa eti kujifunza, Simba na Yanga si vyuo vya wachezaji wa kigeni, eti watoke kwao, waje wahifunze hapa!


Simba:
Justuce Majabvi
Hamisi Kiiza,
Simon Sserunkuma
Juuko Murshid
Pape Nd’aw
Emiry Nimubona
Vicent Agbani

Yanga:
Andrey Coutinho
Mbuyu Twite
Haruna Niyonzima
Thabani Kamusoko
Donald Ngoma
Amissi Tambwe
Vicent Bossou


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic