Nahodha Msaidizi wa Taifa Stars, John Bocco, ataukosa mchezo wa
keshokutwa Jumatano wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Malawi
kutokana na kuwa na majeraha ya kifundo cha mguu, lakini kiungo mshambuliaji wa
timu hiyo, Mrisho Ngassa jana Jumapili alitarajiwa kutua kwa ajili ya mchezo
huo.
Stars ilianza mazoezi Ijumaa ya wiki iliyopita kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar huku Bocco akilazimika kuyakosa mazoezi hayo kutokana na majeraha
yanayomsumbua.
Kocha mkuu wa timu hiyo,
Charles Mkwasa, alisema kuwa wachezaji wote wapo vizuri isipokuwa Bocco
anayesumbuliwa na majeraha ya kifundo cha mguu.
“Amepata mapumziko ya siku tano lakini tunaamini kama atapona
haraka tutamtumia katika mchezo ujao wa marudiano,” alisema Mkwasa.
Kwa upande wa meneja wa timu hiyo, Omari Kapilima, jana Jumapili
aliliambia gazeti hili: “Bocco bado hajaanza mazoezi lakini kwa sasa nipo
njiani kwenda uwanja wa ndege kumpokea Mrisho Ngassa anashuka leo (jana)
mchana, lakini Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wataingia kesho (leo).”
Ikumbukwe kuwa, Ngassa anacheza soka la kulipwa katika Klabu ya
Free State Stars inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini huku Mbwana na
Ulimwengu wakikipiga katika Klabu ya TP Mazembe ya DR Congo.
0 COMMENTS:
Post a Comment