Uongozi wa Simba umeanzisha mfumo wa kuwakata
mishahara wachezaji wote watakaoshindwa kufanya mazoezi pasipo sababu ya msingi
wala kutoa taarifa sehemu husika, jambo ambalo linamaanisha inataka kila mmoja kili
yake iwepo kwa ajili ya kuisaidia timu.
Ni wazi kuwa Simba bado inajijenga
baada ya kupotea kimataifa katika misimu mitatu mfululizo, hivyo inahitaji kuwa
na wachezaji wenye ari ya ushindi kwa timu nzima na wenye nidhamu ya kufanya
mazoezi.
Mratibu wa klabu hiyo, Abass Suleiman ‘Gazza’,
Ijumaa aliwaweka kikaoni nyota wote na kuwaeleza utaratibu huo na kuwataka kila
mmoja anapokuwa na udhuru ni lazima atoe taarifa sehemu husika na kwamba siyo
jukumu la kiongozi kumuuliza mchezaji kwa nini hajafika mazoezini, vinginevyo
wasilaumiane mwisho wa mwezi wakikuta akaunti zao zinapungukiwa.
"Nilitaka kuwaweka wazi, kila
mchezaji atambue kuwa asipokuja mazoezini, hakuna tena kiongozi kuanza
kumtafuta mchezaji kumuuliza sababu za kutofika, badala yake mchezaji ndiye
atoe taarifa kama atakuwa na udhuru. Tumepanga yeyote ambaye atakosa mazoezi
pasipo taarifa sehemu husika, wajibu wangu ni kurekodi watoro na mwisho wa
mwezi tusije kulaumiana akikuta amekatwa mshahara," alisema Ally bila
kufafanua watakuwa wakikata asilimia ngapi kila mchezaji anapokosa mazoezi.
0 COMMENTS:
Post a Comment