MWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombale
Mwiru, jana alitangaza rasmi kujitoa kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
akasisitiza kwamba haendi chama chochote.
Kingunge aliyewahi kutabiri anguko la chama hicho
kikongwe nchini, sasa ana umri wa miaka 85 na ameamua kujitoa CCM ambayo ni
kati ya walioanza nayo baada ya muungano wa Tanu na ASP uliozaa CCM, Februari
5, 1977.
Kingunge aliwahi kuwa mmoja wa memba wa Bunge la
Tanzania kwa vipindi viwili tofauti lakini alikuwa kati ya sehemu kubwa
waongoza mapambano ya CCM ingawa si kipindi hiki.
Wakati Kingunge anatangaza kujitoa, kimekuwa
kipindi ambacho kampeni za vyama zikiwa zimepamba moto na ndiyo maana unaona
leo ni gumzo kuondoka kwa mzee huyo.
Kujitoa kwake, kwetu wanamichezo si ishu sana,
kuliko tungesikia timu yetu ya taifa, Taifa Stars imefuzu kucheza Kombe la
Mataifa Afrika (Afcon) au lile la dunia.
Ndiyo maana wakati wengi wakiwa wametekwa na
suala la kujitoa kwa Kingunge CCM, mimi nikaanza kuwaza miaka yote ile, leo
ameondoka bado Taifa Stars haijafuzu tena Afcon, wala haina mpango na Kombe la
Dunia.
Angalau ingekuwa inaweza kufuzu, Kingunge bado
angeiona akiwa nje ya CCM. Tujiulize kwa sasa Stars ina dalili hata za kufuzu
michuano hiyo mikubwa?
Michuano mikubwa kwa timu yetu sasa ni ile ya
Chalenji ambayo ni michuano ya kanda na mara nyingi inaendeshwa “kimagumashi
tu”. Hatuna kipi hadi tushindwe kufika Afcon au Kombe la Dunia?
Sasa Kingunge ameondoka, anakwenda wapi, anajua
mwenyewe, lakini Taifa Stars haina nafasi ya kufuzu, haina uhakika na hakuna
dalili yoyote kwamba kuna nguvu za dhati mwaka fulani uwekwe kama mpango
madhubuti kwamba iwe isiwe, lazima Stars icheze Afcon au Kombe la Dunia.
Achana na Afcon, Kingunge ameondoka CCM hajawahi
kuiona Taifa Stars ikipata nafasi ya kucheza Kombe la Dunia. Ingawa sijui
anashabikia timu gani, nafikiri hata kama ataenda Ukawa, bado hatapata nafasi
ya kuiona Stars inacheza michuano hiyo mikubwa.
Sina maana Kingunge hataiona Stars ikifika Kombe
la Dunia kwa kuwa ana miaka 85, lakini hata mwenye umri kama wangu, kama
nitaajaliwa kufikia nusu ya umri wa Kingunge bado inaonekana hakuna matarajio
na hatuwezi kuyafikia kwa kuwa kila uongozi unaoingia Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), unaona ni kama jambo gumu sana.
Kama ni jambo gumu sana, haliwezekani, sasa nani
atatusaidia kufuzu? Jibu ni kwamba tutakwama na mambo hayatawezekana kabisa.
Angalia wadau wengine, viongozi kibao wa soka
wanaingia madarakani lakini wanaonekana wamepania kwelikweli kufanikisha
malengo yao binafsi. Najua utaniuliza kwamba viongozi wa klabu ipi na ipi?
Nakukumbusha, nchi yoyote ikiwa na kiwango cha
juu kisoka, au ikauza wachezaji wengi, watakuwa msaada mkubwa katika kikosi
chake cha timu ya taifa na kitakuwa imara sana.
Viongozi wa klabu kama wangekuwa na mikakati,
wakawa na timu bora, zenye ushindani mkubwa Afrika kama ilivyo TP Mazembe,
Enyimba enzi hizo, Al Ahly, Zamalek na nyingine, lazima kungekuwa na kikosi
bora kabisa cha timu ya taifa.
Tunaona Uganda wanavyosaidiwa na wachezaji wengi
wanaocheza nje na angalau wamekuwa na mwelekeo wa ushindani. Hali kadhalika
Kenya angalau wanatangaza jina lao hadi katika Ligi ya England ‘Premier’
kutokana na wachezaji wao. Wamebakiza vitu vichache tu, wakivibadili watapiga
hatua.
Oktoba 7, Taifa Stars inaanza mbio za kuwania
kucheza Kombe la Dunia kwa kuivaa Malawi. Huenda inaweza kuwa nafasi nzuri ya
kumuonyesha Kingunge angalau aingie kwenye bahati ya kuiona Stars ikifanya
vizuri.
Msisubiri arudi CCM ambako amelia ujana wake wote
bila kuinoa Stars ikicheza michuano mikubwa ya kimataifa. Huenda bora kumpa
zawadi ya uzeeni akiwa nje ya CCM na hakuna haja ya kusubiri hadi Kingunge
aamue tena kurudi CCM!
0 COMMENTS:
Post a Comment