Na Saleh Ally
NIKISEMA beki Vincent Bossou, raia wa Togo,
alisajiliwa Yanga kwa kuwa alionekana anamkaba mshambuliaji gwiji wa Ivory
Coast, Didier Drogba, nani anaweza kunikatalia?
Nikikuambia hivi, kwamba kama picha ya
mchezaji akimkaba mchezaji maarufu duniani ingekuwa inatumika kwenye usajili,
basi beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani sasa wangekuwa wanacheza
Ligi Kuu England, unawezaje kunikatalia?
Maana Yondani na Cannavaro wakiichezea Taifa
Stars, wana picha kibao wakipambana na washambuliaji kama Drogba, Salmon Kalou
wa Ivory Coast, Kaka, Robinho, Ramires wa Brazil pia Samuel Eto’o na nyota
wengine wa Cameroon.
Bossou ameonekana ni beki mwenye uwezo, beki
ambaye ataisaidia Yanga tena katika michuano ya kimataifa kwa kuwa alionekana
akipambana na Drogba wakati Togo ikipambana na Ivory Coast.
Lakini hadi sasa, Yanga imecheza mechi tano
ambazo ni dakika 450 mchezaji huyo amekuwa akiendelea kubaki benchi bila ya
kupata hata dakika moja ya kucheza.
Dakika 450 katika benchi kwa mchezaji wa
kimataifa anayetarajiwa kuisaidia Yanga kimataifa akiwa ameshindwa kupata
nafasi ya kuisaidia katika mechi za nyumbani, kweli inaingia akilini?
Analipwa mshahara wa dola 3,000 (zaidi ya Sh
milioni 6), lakini bado yuko benchi na walio chini kimishahara au maslahi ndiyo
wanaoitumikia Yanga. Je, Mtogo huyo ni mradi wa mtu ndani ya Yanga?
Najua wako ambao kamwe hawataki hili liguswe
kwa kuwa wanaona kama wanaingiliwa, wanaona kama wanasakamwa. Swali, Bossou
faida yake kwa Yanga ni ipi na vipi benchi la ufundi lilipitisha asajiliwe?
Bado kilio changu kilekile, klabu zimelialia
kuongezewa wachezaji wa kigeni kutoka watano hadi kumi, TFF na Bodi ya Ligi
Tanzania (TPLB) wakakubali kuongeza wachezaji hadi wafikie saba.
Maana yake katika ile idadi ya tano,
wachezaji wa kigeni sasa wakaongezwa wawili na kufikia saba. Lakini Yanga
imekuwa ikiwaacha wawili benchi katika mechi zote tano ambao ni Bossou na
Andrey Coutinho, raia wa Brazil.
Kumsafirisha mchezaji kutoka Brazil,
unamlipa mshahara wa dola 2,500 (zaidi ya Sh milioni 5 kwa mwezi), lakini
anaendelea kukaa benchi na wanaoitumikia timu ni wale wanaolipwa chini yake,
maana yake nini?
Huenda sielewi maana ya mchezaji wa
kimataifa, tena napenda mnifundishe hasa kwa kuwa kama kweli anakaa nje mechi
tano huku wazalendo ndiyo wakimuonyesha soka linachezwa vipi, hiki ni
kichekesho cha karne!
Nauliza hivi, uongozi wa Yanga unaweza
usisikie uchungu kwa kuwa fedha hizo si mali ya kiongozi yeyote wa utendaji au
kama zinamilikiwa na uongozi basi atakuwa Mwenyekiti Yusuf Manji, hivyo hakuna
anayeona uchungu.
Au benchi la ufundi linaloongozwa na kocha
mkongwe, Hans van Der Pluijm limeamua kukubaliana na hilo, halafu linaona ni
sawa kwa kuwa hakuna kati yao anayelipa mshahara au mwenye uchungu na fedha za
Yanga?
Niulize, benchi la ufundi lilishawishiwa?
Benchi la ufundi lililazimishwa? Kwamba lazima limsajili Bossou au kumbakiza
Coutinho waendelee kubaki benchi?
Kama Yanga ilimuacha beki mzalendo Rajab
Zahir na kumchukua Bossou, tofauti yake au faida yake ni nini hasa?
Hakika kuna mambo yanashangaza na
kuchanganya sana ingawa inaonekana ni kawaida kwa wengine lakini sasa huu ndiyo
wakati Yanga impe nafasi Bossou acheze, aache tu kushuhudia mechi za Yanga
akiwa amekaa kwenye kiti huku akilipwa mamilioni.
Nasisitiza kama Coutinho na Bossou hawana
uwezo hata wa kucheza kikosi cha kwanza kwa mechi tano, yaani dakika 450, Yanga
lazima ifanye uamuzi mgumu na kama ni mradi wa mtu, sasa ndiyo wakati sahihi wa
kuusambaratisha. Nitarudi.
FIN.
0 COMMENTS:
Post a Comment