October 19, 2015


Na Saleh Ally
ELIUS Mrugau Maguli ameifungia timu yake ya Stand United mabao matano, ikiwa inacheza kwenye uwanja wake wa Kambarage ulio katika Kitongoji cha Majengo katika Manispaa ya Shinyanga.

Maguli amefunga bao moja wakati Stand United ikicheza nje ya Shinyanga. Alifunga bao hilo katika mechi ya pili ya Stand United wakati ikicheza na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Ukitaka jumla, mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba, amefikisha mabao sita na ndiye anaongoza kwa ufungaji mbele ya wachezaji wa kigeni kutoka Yanga, Simba, Azam FC.

Maguli ambaye anaongoza kwa kufunga mabao mbele ya wachezaji wote wazalendo, amefunga mabao manne katika kipindi cha kwanza kupitia dakika za 6, 19, 23 na 33. Mawili amefunga katika kipindi cha pili ambayo ni dakika za 47 na 54.


Unaweza kusema mgawanyo wa mabao yake kwa maana ya wakati gani, tayari ni mshambuliaji anayeweza kufunga mabao katika kipindi cha kwanza, pia cha pili. Lakini anaweza kufanya hivyo akiwa nyumbani au ugenini.

Bado inaonyesha hivi; Maguli amefunga katika mechi nne kati ya saba ambazo Stand United wamecheza nyumbani na ugenini.

Tena inaonyesha hivi; Maguli amefunga mara mbili mabao mawili wakati Stand United ilipoichapa African Sports kwa mabao 2-0 mjini Shinyanga, halafu akafanya hivyo waliposhinda kwa mabao 3-0 dhidi ya Prisons ndani ya Kambarage.

Inaonyesha hivi, mabao pekee ya Maguli yameisaidia Stand United kubeba pointi 12, wakati yenyewe ina pointi 12 katika nafasi ya tano.


Mechi dhidi ya African Sports walishinda 2-0, akafunga yote, wakashinda 1-0 dhidi ya JKT, mfungaji pekee ni yeye, wakaitwanga Mbeya City 1-0, muuaji ni Maguli, juzi wameilamba Prisons 3-0, ‘kaingia’ nyavuni mara mbili.

Pointi 12 zote za Stand United lazima umhusishe Maguli. Kwamba ndiye mhimili sasa wa ushambulizi katika kikosi cha Stand United kinachofundishwa na Mfaransa, Patrick Liewig.

Ukisoma vizuri maelezo hayo, utagundua Maguli ni kati ya washambuliaji bora kabisa ambao hata timu zetu kubwa zilikuwa zinawahitaji. Mfano zile zinazoshiriki michuano ya kimataifa kama Yanga na Azam FC.

Wakongwe wengine kama Simba ambao wanataka kurejea katika heshima yao, pia watakuwa wanahitaji mtu kama Maguli.

Maguli ana mabao sita, sawa ligi haijaisha, kweli ndiyo mbichi kabisa lakini ndiye mshambulizi hatari zaidi kuliko wageni na wazalendo wote kwa kipindi hiki.



Hilo halina ubishi, lakini hapohapo, huenda ndiyo wakati mzuri na mwafaka kujifunza. Kwamba ndani ya kikosi cha Simba, unapozungumzia suala la usajili, Kamati ya Usajili chini ya Zacharia Hans Poppe au ile ya ufundi pamoja na benchi la ufundi, wana tatizo la kujua washambuliaji bora?

Unakumbuka walimuondoa Amissi Tambwe, wakasema Kocha Patrick Phiri ndiyo amesema hivyo? Yeye akasema hapana, hawezi kumuondoa mshambuliaji bora wa msimu uliopita. Viongozi wakaendelea kusisitiza Phiri ‘amewaingiza chaka’.

Hilo likapita, sasa limeiva suala la Maguli, ameondolewa Simba katika hali ya kushangaza, imeshitua wengi kwa kuwa bado Simba haikuwa imekaa vizuri katika safu ya ushambuliaji na ilihitaji mtu kama Maguli na tayari ilikuwa naye.

Maguli kaondoka, Simba imemsajili mshambulizi ‘mtalii’, Pape N’daw, raia wa Senegal ambaye hadi sasa ‘anauza sura’ tu. Taarifa zinaeleza huyo ndiye chaguo la Kocha Dylan Kerr na mwingine aliyehusika kumshauri ni Collins Frisch mjumbe wa kamati ya utendaji ambaye ni sehemu ya kamati hizo mbili. Sasa N’daw na Maguli ambaye ni mzalendo, yupi ni msaada kwa Simba?


Baada ya mechi sita, Simba imefunga mabao nane, kati ya hayo matano yamefungwa na Kiiza. Utaona Maguli ana mabao sita, anazidiwa mawili tu na kikosi cha Simba lakini hakuna mtu anayeweza kumfikia katika kikosi hicho.

Kamati ya usajili na kamati ya ufundi, kweli wao kila wakati ni watu wa kuingizwa ‘chaka’ kama ilivyotokea kwa Phiri na sasa Kerr anayeendelea kupiga debe kwamba N’daw atakuwa ni msaada kwa Simba!

Tujiulize, kweli watu wa kamati hawana uwezo wa kufikiri, kuchanganua na kufanya uamuzi sahihi na badala yake wataendelea kuingizwa chaka hivyohivyo na kuziachia timu nyingine washambulizi bora wakati ligi inaendelea?

Kama sivyo, basi kamati zenyewe zitakuwa na watu wasio makini ndani, huenda wanaoamua kwa kufanya mambo kishabiki, kwa ubinafsi, ikiwezekana chuki au hawajui mambo, ili mradi wanaungaunga tu!

Mafanikio ya Maguli ni aibu nyingine kwa Simba, kamwe hawaikwepi na haina tofauti kubwa na ile ya Tambwe ambaye aliondolewa akiwa mfungaji bora msimu mmoja kabla na sasa ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kama utajumlisha misimu miwili ya 2013-14 aliokuwa mfungaji bora akitupia mabao 19 na ule wa 2014-15 aliopachika mabao 14.

Kuna kila sababu sasa watu hao wa Simba waache ubishi, hata kama wanajua sana, basi wajifunze kupitia makosa na si kuendelea wao kuwa makosa.

MECHI:
Stand                   2-0         A. Sports             Kambarage
Elius Maguli 19
Elius Maguli 33

 JKT Ruvu           0-1         Stand                   Karume
                                         Elius Maguli 6

 Stand    1-0         Mbeya                 Kambarage
Elius Maguli 47

Stand    3-0         Prisons                Kambarage
Elius Maguli 23
Elius Maguli 54


WAFUNGAJI WANAOONGOZA LIGI KUU BARA:
 Elias Maguli Stand                    6          
Hamisi Kiiza           Simba         5          
Donald Ngoma        Yanga        5          
Tambwe                    Yanga        4          
Tchetche                  Azam          4          
Atupele Green         Ndanda     3          
Miraji Athumani    Toto            2          
Fully Maganga        Mgambo    2          
Busungu                   Yanga         2          
Ali Manzi                  Prisons      2          
Jeremiah Juma      Prisons      2          
Edward Christopher Toto        2


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic