October 26, 2015


Na Saleh Ally
NILISIKIA mjadala mkubwa umeanzishwa na mashabiki wa soka ambao walikuwa wamemaliza kusikiliza kipindi cha redio cha E Sports kinachorushwa na E FM Radio.


Mashabiki hao wa soka walikuwa wamemaliza kumsikiliza Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye alikuwa akihojiwa kuhusiana na timu yake kupaya ushindi.

Julio alieleza waliofunga mabao, akaeleza moja limefungwa na Jerry Tegete umbali wa mita 30 hivi. Tena kwa mbwembwe Julio akasisitiza kwamba kama ataendelea hivyo, basi ataweza kurejea timu ya taifa.

Mchambuzi mmoja wa EFM aliyekuwa studio siku hiyo, huenda ndiye alisababisha mjadala huo baada ya kusema Julio ana haraka sana na si jambo lahisi kurejea kikosini Stars.

Mjadala ule ulinivutia, wako walimuunga mkono mchambuzi yule na wengine wakakataa kabisa. Mimi nikabaki upande wa pili, kwamba kweli Tegete anaweza kabisa kurejea kikosini Taifa Stars.
 

Siku chache baadaye, Tegete akafunga mabao mengine mawili. Ndani ya mechi hizo mbili akawa amefunga mabao matatu, kaanza kuwa gumzo.

Mnitakurudisha nyuma kidogo; wakati Fulani niliwahi kuandika na kumchambua Tegete nikihoji huyu mtu imekuwaje anaendelea kubaki Yanga ‘akichezea’ benchi wakati kocha Hans van der Pluijm alishaonyesha wazi hakuwa anamhitaji tena.

Niliona Tegete alikuwa akipoteza muda wake na alistahili kuondoka na kwenda kuanza upya. Kama Yanga wanamhitaji, basi siku nyingine na kama haiwezekani, atajua huko mbele.

Nilieleza kiasi gani alivyo na uwezo mkubwa wa kufunga. Tegete ni muuaji hasa, muite ‘Killer’ anapoliona lango, zaidi ya asilimia 80, huwa hafanyi utani.

Inawezekana kabisa akawa ndiye Mtanzania mwenye uwezo mkubwa wa kumalizia landoni katika kipindi hiki. Lakini niliona hakuwa makini na hakuwa akijitambua.

Wakati baadhi wakipongeza makala hayo na wengine wakilala. Tegete alinipigia simu, akanieleza maneno ya kushangaza sana. Niliamini tayari ana nafasi ya kurejea tena na kuwa bora na si ajabu ukisikia Yanga wameanza kumlilia tena arudi Jangwani.

Tegete alinipigia simu na kusema hay: “Anko nimesoma makala yako, naomba nikuambie nimeelewa. Kweli nilikuwa nalifikiria hilo, lakini nilikosa ujasiri wa kuanza. Nakuahidi nitafanya hivyo utaona.”

Tulizungumza mengine, pia nikamalizia kwa kumtia moyo. Siku chache baadaye nilisikia ameanza mikakati ya kutafuta timu kabla ya kuangukia Mwadui FC.

Mwanzoni sikumsikia akifunga, lakini sikuwa na hofu kwa kuwa nilijua anahitaji muda. Lakini kama atakuwa mzima wa afya, fiti na aliyerejea katika hali ya kujitambua kweli, hakika ni vigumu sana kumzuia asifunge mabao 10 au zaidi katika msimu mmoja.

Bado Tegete anahitaji kuizoea Mwadui FC, anahitaji kuzoea mazingira na mwendo wa Julio na wengine katika benchi la ufundi. Lakini baada ya hapo ni kazi ngumu kumzuia muuaji huyo, nasisitiza muite Killer.

Unajua namna Taifa Stars inavyohaha suala la wafungaji. Tuna wawili Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta wanaocheza nje. Lakini tuna John Bocco, lakini washambuliaji wazuri watatu kwa taifa hawatoshi.

Acha Tegete arudi, ninaamini kazi yake itaonekana na kweli kama ataendelea kujituma. Hakuna mwenye uwezo wa kuzuia kasi yake ya ufungaji kwa kuwa kama binadamu wana vipaji vingi, basi Tegete amepata bahati, mwenyezi Mungu kamjaalia kujua ‘kucheka na nyavu’.

Kipaji alichonacho Tegete kitabaki kuwa msaada kwa taifa letu kwa kuwa licha ya kuisaidia Mwadui atakuwa msaada kwa Taifa Stars. Ninakubaliana na Julio, kweli akiwa makini, hakuna wa kumzuia Killer kurejea tena Stars.

Karibu tena anko, uliondoka kwa uzembe wako, umerudi kwa akili zako. Kiti chako bado kipo, hakuna aliyekikalia. Kila la kheri.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic