October 26, 2015


Na Saleh Ally
KAMATI ya Usajili ya Simba ilijifunza mambo mengi sana kuhusiana na matatizo ya usajili. Unakumbuka mamgo yalivyokwenda kwa kubahatisha msimu uliopita.


Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe baadaye akaeleza kuhusiana na suala kama wakifeli, lawama haziwezi kwenda kwao pekee.

Alieleza namna wanavyoshirikiana na kamati ya ufundi, pia ushirikiano wao na kamati ya utandaji unavyokuwa.

Hivyo kama watafanya vizuri pongezi ni kwa wote na kama wakiboronga, basi ni kwa wote pia.

Sasa unaona hii inayofuatia kutoka kwangu si lawama, badala yake mshangao namna mambo yanavyokwenda. Kwamba Simba imefunga mabao nane na kati ya hayo, saba yamefungwa na wageni.

Wachezaji wa ushambuliaji na safu ya kiungo cha ushambuliaji ukianzia na Mussa Hassa Mgosi, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Joseph Kimwaga na Boniface Maganga.

Simba imefunga mabao nane katika michezo sana ambayo yamefungwa na Hamisi Kiiza (matano), Justice Majabvi, Juuko Murshid (kila mmoja bao moja) na Mtanzania mmoja ambaye ni Kimwaga.

Utaona kiasi gani namna ambavyo Wazalendo wamelala na kushindwa kufanya lolote kuisaidia Simba na hawaonyeshi ushindani sahihi.

Inawezekana hawa wanajua kwamba Simba inahitaji nini au wanaweza kuhoji inakuwaje lazima wafunge tu wanaweza kuisaidia timu ushindi. Kama ni hivyo wamefanya hivyo lini?

Simba inahitaji mabao ambayo ndiyo yatakuwa yakiipatia ushindi. Kama wachezaji watafunga, kwa lugha nyepesi ni kuisaidia timu kushinda.

Kila mchezaji wa Simba nikianza na wazalendo, lazima ajime, msaada wake kwa timu hiyo umekuwa upi.

Mtendaji mshindani lazima hujiuliza, kama umefika wakati wa malipo, yaani mshahara anapoanza kudai, alikuwa na mchango upi.

Mtu mwenye tabia ya ushindani, anayetaka anachokitumikia kifanikiwe lazima ajiuliza kuhusiana na mafanikio au msaada anaotoa kwa kile kinachompa mshahara.
Kama mwajiriwa anapokea tu mshahara, hataki kujua kama ametoa nini kwa mwajiri wake, basi pia ni tatizo na anaingia katika kundi la binadamu wanaokwenda kwa mwendo wa kubahatisha.

Niwe wazi, wazawa wa Simba hasa walio katika safu ya ushambuliaji hawana mwendo mzuri na ikiwezekana wanakwenda kwa mwendo wa kubahatisha ambao si sahihi hata kidogo.


Hata nikisema hawana msaada bado itakuwa sawa. Nikisema hawana mapenzi ya dhati na Simba naamini pia nitakuwa sahihi kwa kuwa kweli hawasaidii lolote.

Inawezekana kabisa hata ndani ya kikosi wakawa hawapendani, wanaoneana wivu ndiyo maana mwendo unaweza usiwe bora.

Simba imetoa ajira kwao, lakini hawaonyeshi uwezo sahihi na hatujasikia wakilia na mishahara au wakilalama kutolipwa stahiki zao jambo ambalo linaonyesha ni watu wasiostahili kupewa jukumu la kuutetea ukubwa wa Simba.

Viongozi wamekuwa wakikosea tunawasema bila ya woga hata kidogo. Ninajua wamekuwa wakikasirika, lakini kwa kuwa lengo ni kukuza soka nchini, nitaendelea kusema bila ya woga.

Leo nimehamia kwa wazawa ambao wanaonekana wako doro, wamelala na ikiwezekana wala hawajali tena wanaona kuchezea Simba, basi ndiyo mwisho.

Mgosi alifanya vema Mtibwa Sugar, vipi sasa amerejea Simba ndiyo kama amelala vile na kila kitu kimeisha?

Lakini hawa vijana, mfano Ajibu aliyefululiza kufunga hat trick ikaonekana Simba wamepata ‘mtu’, vipi sasa, yuko wapi, anafanya nini na msaada wake kwa Simba ni upi?

Wazawa achene mambo ya hadithi, kulalama na kuendelea kuwepo bila ya kujua kwamba muda unakwenda na kufanya vibaya kwa kikosi kunakuwa juu yenu pia.

Kocha ana kazi yake, lakini hamuwezi kukwepa kwamba kama Simba inalala, basi ndiye ndiyo tatizo na mnawajibika fanyeni kazi achene longolongo.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic