Na Saleh Ally
RAIS wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
amezungumza mambo mengi sana mazuri wakati wa sherehe wa kukabidhiwa tuzo
maalum na Chama cha Waandishi wa Habari wa Michezo (Taswa) zilizofanyika kwenye
Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, juzi.
Kikwete alipewa tuzo kutokana na mchango
wake mkubwa katika michezo katika kipindi chake cha uongozi kwa miaka 10 ambacho
kinafikia tamati mwezi huu.
Hakuna anayeweza kulikataa hilo, hata
kama haukuwa mchango wa kutosha, lakini si haba, alijitahidi.
Wakati wa mkutano huo, akitoa hotuba
yake, Kikwete aliwavutia watu wengi sana kwa kuwa alizungumza vitu vingi
kuhusiana na michezo ndani na nje ya Tanzania. Wengi wakawa wakisema
chinichini: “Jamaa mfuatiliaji, kweli anaijua michezo.”
Kikwete ni mwanamichezo hasa, ndiyo
maana amekuwa tayari kuwalipia makocha wa timu za taifa za soka, riadha,
netiboli na kadhalika na alieleza sababu ya kufanya hivyo kwamba kuwapa watu
mwalimu ni zawadi kubwa.
Wakati Kikwete anazungumza kuhusiana na
kocha, alieleza namna ambavyo Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa
anavyofanya kazi na kusema ameanza vizuri kwa kuing’oa Malawi katika kuwania
kucheza Kombe la Dunia 2018.
Pia akasisitiza kwamba Tanzania
inakutana na Algeria ambayo ina wachezaji wakali hasa na inahitaji juhudi ya
uweledi kupambana nao na kuwang’oa kwa kuwa wakati wa Kombe la Dunia mwaka 2014
nchini Brazil, Algeria ilimaliza michuano hiyo ikiwa timu bora ya Afrika. Kweli
Kikwete ni mfuatiliaji.
Lakini akasisitiza kwamba mshahara
alioutoa wa kocha wa Taifa Stars, hakuwahi kusema alipwe hadi atakapokuwa
mzungu au raia wa kigeni, maana yake hapa, Mkwasa apewe mshahara wake.
Mshahara anaotakiwa kulipwa Mkwasa ni Sh
milioni 25 kwa mwezi ndicho alichotoa Kikwete. Sasa vipi inaonekana kumeanza na
uzungushwaji wa mambo.
Hata kabla Mkwasa hajaingia mkataba na
TFF, kulionekana kuna figisu zinatembea. Nilianza kufanya uchunguzi na kugundua
kwamba suala la mshahara wa kocha huyo linakwama katika Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo.
Nilizungumza na ofisa mmoja wa wizara
hiyo ambaye alisema kwamba wanashughulikia ingawa hakutaka ifanywe habari. Bado
hawakuwa wamekubali kuutoa mshahara huo hadi Kikwete ameamua kuzungumza.
Nafikiri sasa siyo siri tena, wanapaswa
kumlipa Mkwasa mshahara wake wa nyuma, wamlipe baada ya kuingia mkataba na pia
stahiki kama nyumba wampe.
Kocha Kim Poulse kutoka Denmark, alikuwa
akiishi Masaki, hali kadhalika Mart Nooij ambaye alikuja ‘kufanya utalii’
Tanzania. Sasa angalau Mkwasa ameanza kuonyesha njia. Kwa kuwa ni mzalendo
ndiyo hastahili kupata lolote?
Watanzania tunapenda kujidharau, huenda
kutoka wizarani kwenda kumlipa kocha wa Kizungu kama Poulsen au Nooij
ilionekana ni jambo la kawaida na huenda anayehusika na ulipaji
aliona ni jambo zuri sana.
Kwa kuwa sasa ni mzalendo, basi
mizunguko inakuwa mingi. Taarifa nyingine za uchunguzi zinaonyesha hata funguo
za nyumba zinashikiliwa wizarani. Sasa huu ndiyo wakati mwafaka, nazo apewe kwa
kuwa ni haki yake.
Kauli ya Kikwete kwamba alitoa mshahara
kwa ajili ya kocha wa Taifa Stars bila ya kujali ni Mtanzania au la inaonyesha
kiasi gani yeye anaweza kuwaamini makocha wazalendo.
Mkwasa si Mungu, kama ni binadamu naye
siku itafikia atakosea, na hatutasita kumueleza. Lakini kwa sasa, mimi
naendelea kusimama mstari wa mbele kwa kuwa nilishaanza, apewe haki zake ili
tuonyeshe tunawajali na kuwathamini wanamichezo wazalendo wa hapa nyumbani.
Wanaohusika na malipo ya kocha huyo,
watimize hilo kwani hata anayetoa amelipita hilo tena kwa kuonyesha heshima kwa
Watanzania. Sasa anayetaka kuzuia ni nani?
Angalizo, si kwa kuwa Kikwete anamaliza
muda wake, basi ndiyo iwe nafasi ya kutaka kulizungusha hilo hadi lishindikane.
Kama kuna ambaye alikuwa hataki kumlipa, basi amlipe ili iwe sehemu nyingine ya
motisha kwake.
Mechi dhidi ya Algeria ni ngumu, msimpe
nafasi Mkwasa apate kisingizio. Tafadhari mumlipe fedha yake kwa wakati mwafaka
maana aliyejitolea kumlipa, ameshaweka mambo hadharani.
0 COMMENTS:
Post a Comment