RODGERS |
Ikiwa zimepita siku chache tangu uongozi wa Liverpool ya England,
umtimue kocha wake, Brendan Rodgers, kocha wa Simba ambaye ni rafiki wa
Rodgers, Dylan Kerr, ameibuka na kusema kuwa kitendo hicho kimemuuma, japo
kulikuwa hakuna namna.
Kerr na Rodgers walikuwa marafiki wakati walipokuwa katika timu ya
Reading ya England, wakati huo Kerr akiwa mchezaji anayeitumikia nafasi ya beki
wa kushoto huku Rodgers akiwa mfanyakazi wa timu hiyo.
Kerr alisema kuwa baada ya
kusikia taarifa hizo za swahiba wake kutimuliwa, zilimuumiza kwa kiasi kikubwa
japo anaona kulikuwa hakuna namna ya Rodgers kukwepa janga hilo.
“Ni kweli nilipata taarifa za rafiki yangu Brendan Rodgers
kutimuliwa ndani ya Liverpool ambapo taarifa hizo zilikuwa mbaya mno kwa upande
wangu.
KERR |
“Lakini jambo hilo kwa hakika lisingewezakana kuepukika kwake
kutokana na kushindwa kuijenga klabu hiyo ndani ya misimu mitatu ambapo katika
kipindi hicho pia aliwauza wachezaji muhimu, hapo utaona lazima timu iyumbe.
“Suala hilo ndilo naona limechangia kutimuliwa kwake, lakini jana (juzi)
nilimtumia ujumbe wa kumpa pole kutokana na kupoteza kibarua chake hicho,” alisema
Kerr.
Ikumbukwe wakati pazia la Ligi Kuu Bara linafunguliwa Septemba, 12
mwaka huu, Rodgers alimtumia ujumbe wa kumtakia mafanikio mema Kerr katika
msimu wake wa kwanza akiwa na Simba.
0 COMMENTS:
Post a Comment