Hofu kubwa imetanda ndani ya kikosi cha
Yanga kutokana na hivi karibuni kukumbwa na wimbi la majeruhi wakati
ikikabiliwa na mchezo mgumu ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui FC utakaofanyika
Jumatano hii kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Miongoni mwa wachezaji ambao wamekumbwa na
majeraha ni Amissi Tambwe na Kelvin Yondani.
Hata hivyo, Tambwe na Yondani licha ya kuwa
majeruhi, wameondoka na kikosi cha timu jijini Dar na kwenda Shinyanga tayari
kwa kuivaa Mwadui FC, lakini haijulikani kama watakuwa fiti kwa ajili ya mchezo
huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Inadaiwa majeraha hayo waliyapata katika
mchezo wa ligi kuu dhidi ya Toto Africans ya Mwanza uliofanyika Jumatano
iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuwafanya washindwe
kufanya mazoezi ya nguvu na wenzao hivi karibuni kabla ya jana kwenda mkoani
Shinyanga.
Hali hiyo inamnyima usingizi kocha mkuu wa
timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm ambaye jana kabla ya safari hiyo ya
kwenda Shinyanga, aliliambia gazeti hili kuwa hajui kama anaweza kuwatumia
katika mechi hiyo na anachosubiri ni taarifa ya daktari wa klabu hiyo, Shecky
Mngazija.
Alipoulizwa Mngazija kuhusiana na hali ya
wachezaji hao, alisema kuwa wanaendelea vizuri kwani mamuvu yaliyokuwa yakiwakabili
yalikuwa ni ya kawaida na Mungu akipenda kufikia Jumatano watakuwa fiti na
tayari kwa kupambana na Mwadui FC.
“Hivi
sasa wanaendelea vizuri na tayari wameshaanza kufanya mazoezi mepesi baada ya
kuwapatia tiba, hivyo ni matumaini yangu kuwa mpaka kufikia Jumatano watakuwa
fiti kwa asilimia mia moja.
“Yondani alikuwa anahisi maumivu ya nyonga
na Tambwe alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya msuli wa mgongoni, baada ya
kupatwa na hali hiyo niliwapumzisha kwa
muda ili niweze kuwapatia tiba na sasa wapo vizuri, hivyo kocha asiwe na shaka
yoyote, uamuzi wa kuwatumia au kutowatumia utakuwa ni wake,” alisema Mngazija.
0 COMMENTS:
Post a Comment