Uongozi wa Mbeya City upo katika hatua za mwisho za kukamilisha
ripoti yao na kuipeleka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na
kitendo alichofanyiwa kiungo wa timu hiyo, Joseph Mahundi na beki wa Simba,
Mganda, Juuko Murshid cha kumpiga kiwiko na mwamuzi kutochukua hatua yoyote.
Kitendo hicho kilitokea katika mchezo wa Mbeya City na Simba
uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Oktoba 17, mwaka huu. Juuko alimpiga Mahundi kiwiko wakati hana mpira na mwamuzi hakuchukua
hatua yoyote.
Katibu wa timu hiyo, Emmanuel Kimbe, alisema kitendo kile kiliwasikitisha
kama klabu, ndiyo maana wameamua kuchukua maamuzi ya kupeleka malalamiko sehemu
husika.
Kimbe alisema kuwa katika mchezo ule ambao timu yake ilifungwa bao
1-0 lililofungwa na Juuko, kulikuwa na mambo mengi ambayo yalikuwa si ya kiungwana.
“Kitendo alichofanya beki wa Simba yule Mganda hakikuwa cha
kiungwana kabisa na sisi tumeona hakuna hatua iliyochukuliwa na mwamuzi na
wahusika wapo kimya, tulichoamua sisi ni kuandika barua ikiwa na vielelezo
vyote pamoja na video ya tukio kwa TFF.
“Kwa sababu siku ile yalitokea matukio mengi lakini yalikuwa yanafumbiwa macho, hivyo na
sisi hilo hatulipi nafasi, maana Nyosso aliadhibiwa mapema, kwa nini wengine
wacheleweshwe wakati matukio yapo wazi kabisa?” alilalama Kimbe.
0 COMMENTS:
Post a Comment