Straika wa Yanga, Malimi Busungu, ametakiwa kuongeza bidii mazoezi ikiwa ni
pamoja na kugonga msosi wa kutosha kila siku ili aweze kurudisha stamina yake
kama ilivyokuwa hapo awali wakati akijiunga na timu hiyo akitokea JKT Mgambo ya
Tanga.
Busungu ambaye hivi karibuni amejihakikishia
nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kinachofundishwa na Mholanzi,
Hans van Der Pluijm, ameanza kupoteza stamina, jambo ambalo linafanya awe
anadondoka kila wakati uwanjani anapowania mpira.
Kutokana na hali hiyo, Pluijm kwa
kushirikiana na daktari wa timu hiyo, Shecky Mngazija, wamemtaka Busungu
kuhakikisha anajituma zaidi mazoezi ikiwa ni pamoja na kugonga msosi wa nguvu
ili aweze kurejesha makali yake kama ilivyokuwa hapo awali.
Busungu alisema kuwa viongozi wake hao wamempatia
ushauri huo hivi karibuni na tayari ameshaanza kulifanyia kazi.
“Hata kabla ya viongozi wangu kuniambia
hivyo, hali hiyo nilikuwa tayari nimeshaiona, hata hivyo tayari nimeanza kuifanyia
kazi na ninaamini baada ya muda mfupi nitakuwa fiti zaidi ya nilivyokuwa
awali,” alisema Busungu.
Alipoulizwa ni kitu gani kimesababisha apoteze
stamina yake ya awali, alisema: “Inawezekana ni majeraha niliyopata hivi
karibuni lakini nitahakikisha narudisha makali yangu ndani ya kipindi kifupi.”
0 COMMENTS:
Post a Comment