Katika kuhakikisha safu yake ya ushambuliaji
inafunga mabao mengi, Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, ameanza kutengeneza
mbinu mbalimbali zitakazowapa mabao mengi katika Ligi Kuu Bara.
Simba imefunga mabao saba katika mechi tano za
ligi kuu msimu huu lakini bado kocha huyo amekuwa akiona safu yake ya
ushambuliaji haina makali.
Katika mazoezi ya jana kwenye Uwanja wa Boko
Veterani jijini Dar es Salaam yaliyoanza saa 3:00 asubuhi hadi 11:00 asubuhi,
mbinu zilizotawala zilikuwa za kufunga.
Programu hiyo, iliwahusisha wachezaji wote
wakiwemo mabeki, viungo na washambuliaji ambao ni Mussa Mgosi, Joseph Kimwaga,
Pape Nd’aw na Danny Lyanga.
Awali aliwataka wachezaji kukimbia mbio fupi
wakizunguka nusu uwanja, akahamia katika zoezi la kupiga pasi na kisha akaanza
kutoa mbinu za kufunga.
Kerr aliwataka mabeki wa pembeni, Hassan Kessy,
Emily Nimubona na viungo wa pembeni Simon Sserunkuma na Awadh Juma kuwapigia
krosi wachezaji kwa ajili ya kufunga mabao.
Baadaye Kerr alianza kutoa mbinu za kufunga mabao
nje ya mita 18 na mita 20 ambapo alikuwa akiwatumia viungo kuwatulizia mipira
mirefu.
Baada ya mazoezi, Kerr alisema: “Nahitaji
kuongeza makali ya kufunga, ndiyo maana naongeza mbinu kila siku.”
0 COMMENTS:
Post a Comment