October 12, 2015


GUMZO sasa katika soka nchini ni Kocha Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi kukubali kuchukua nafasi ya Kocha Msaidizi ndani ya Yanga timu ambazo zinacheza ligi moja!

Mwambusi sasa anakuwa msaidizi wa Kocha Hans van Der Pluijm, ambaye alikuwa kocha wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana na kipa wa zamani wa timu ya taifa ya Uholanzi.

Kila mmoja anazungumza lake analoliamini, wengine wakitoa mifano ya Ulaya kwamba haiwezekani, jambo ambalo ni sahihi. Lakini wamesahau namna ambavyo Tanzania inavyowezekana kutokana na mambo kadhaa kama haya yafuatayo.

Maslahi:
Ndiyo, suala la maslahi ni muhimu sana ingekuwa Ulaya, Mwambusi asingekubali kweli kwenda Yanga kwa kuwa ni kocha mkuu.

Lakini hapa Tanzania, hii si mara ya kwanza na huenda likawa funzo kubwa.

Kwamba kocha msaidizi wa Yanga, ana mshahara mara mbili na ushee wa kocha wa timu nyingine mfano Mbeya City, Coastal Union au nyingine.

Mwambusi ana familia kama sisi, ana majukumu na huenda angependa kuona familia yake inaishi kwa raha zaidi.
Hivyo huo ni moja ya msukumo. Maslahi ya Yanga, pia huduma kama nyumba bora, usafiri ni kati ya mambo yaliyomvuta. Lazima tukubali naye ni mwanadamu.

Kila kitu City:
Mwambusi anajua mengi sana kuhusiana na Mbeya City. Mwenendo wa kikosi, wanakwenda wapi na nini kitafuata.

Ana uwezo wa kujua njia wanayopita na mwisho wao kutokana na hali ilivyo. Lazima tukubali ndani ya klabu hizi kuna mengi yanapita chini kwa chini yawe ni ya furaha au karaha, lakini walio ndani kama vile Mwambusi, wanajua mengi zaidi.
Ndiye aliyeipandisha daraja, akaipa nafasi ya tatu, sasa anajua msimu huu utakuwa vipi.

Kama ni hivyo, bado angeweza kubaki kweli na kuisaidia, lakini si vibaya kuondoka kama umepata nafasi ya kujifunza zaidi kwa kuwa Yanga kutakuwa na changamoto kubwa zaidi kutokana na ukubwa wa timu yenyewe ambayo pia inashiriki michuano ya kimataifa.


Ligi ya Mabingwa:
Kama nilivyoeleza mwanzo, Mwambusi anaujua undani zaidi wa Mbeya City kuliko mimi na wewe. Lazima anajua nini kinafuata na hali ikoje, pia nafasi ya kikosi chake kubeba ubingwa.

Kama hawezi, basi anahitaji nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf). Yanga watashiriki, yeye akiwa kocha msaidizi atapata nafasi ya kujifunza mengi.

Hii itamsaidia hapo baadaye kwa Yanga, Simba au timu nyingine yoyote kumuamini kama inashiriki michuano ya kimataifa kwa kutumia rekodi zake, wakati akiwa Yanga.

Uhusiano:
Uhusiano kati ya Mwambusi na Mbeya City, tayari ulikuwa na doa. Walisigana hadi kocha huyo akajitoa katika kikosi.

Juhudi zikafanyika kumrudisha, akarejea. Pamoja na hivyo, hauwezi kujua alifanya hivyo yaani kurudi huenda kwa heshima ya baadhi ya watu au kuonyesha yameisha tu akisubiri ikifika siku, ataondoka zake.

Ana haki ya kufanya hivyo, kufanya kwake kazi ya juhudi haikuwa pekee anataka kuonekana au sura yake iwe maarufu sana. Alitaka afanikiwe kweli na maslahi au kufundisha timu kubwa kama Yanga ni sehemu ya ndoto zake.

Jikoni:
Kujiunga na Yanga kama kocha msaidizi ni sehemu ya kusogea jikoni. Siku Yanga imeamua kumwamini kocha Mzalendo, huenda Mwambusi akawa wa kwanza kwa kuwa atakuwa yuko tayari kikosini. Kwa rekodi zake za Mbeya City na Moro United, zitamsaidia kupewa nafasi hiyo na huenda akafanya vizuri zaidi.

Inashangaza wengi kuona Mwambusi akiwa kocha mkuu anayeiacha Mbeya City na kuwa kocha msaidizi Yanga.
Lakini hakuna anayeshangaa aliyekuwa kocha msaidizi Yanga, amepewa timu ya taifa na kuwaacha makocha wakuu 16 wa Ligi Kuu Bara wakiwa hawana nafasi ya kuifundisha timu ya taifa.

Kocha msaidizi, ndiye kocha mkuu pia. Maana ndiye msaidizi wa bosi mwenye nafasi ya kuwa kocha mkuu wakati wowote.

Mwambusi anaweza kuwa amekosea kwa maana ya mtazamo, lakini uamuzi wake ukawa umemtengenezea ushujaa wa baadaye na huenda wengine watakuwa wamesahau kabisa.

1 COMMENTS:

  1. Mwambusi hajakosea, yuko sahihi na uamuzi sahihi kwasababu watu wote tuanaagalia maslahi kwanza status baadae! Yanga, Azam na Simba ni kubwa mno kwa Mbeya city na wengineo.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic