Kiungo nyota wa Azam FC, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, amefunguka kuwa licha ya timu nyingine
za Ligi Kuu Bara kuwa ngumu zaidi msimu huu lakini mwendo wa Yanga, unamtisha
na kudhoofisha matumaini yao ya kuchukua ubingwa wa ligi safari hii.
Sure Boy amekiri
kuwa msimu huu pia upo tofauti na msimu uliopita ambapo changamoto ya timu za
juu ilikuwa zaidi kwa Yanga lakini sasa hivi hata Simba nao wameamka na
wamepania kufanya kweli, hivyo kuzidi kuzidisha ugumu wa ligi hiyo na kuifanya
isitabirike mapema.
Aidha, kuhusiana
na mchezo wao wa wiki ijayo dhidi ya Wanajangwani hao, Sure Boy alisema ni
mchezo mgumu na hawezi kutoa matokeo mapema kwa maana anajua Yanga wamejiandaa
hivyo na wao watahakikisha wanakuwa vizuri kwa ajili ya kutafuta pointi tatu
muhimu.
“Aisee, hii ligi
ya safari hii ngumu sana, hata msimu uliopita haikuwa hivi, hii ya sasa
haitabiriki maana kama unavyoona Yanga imeng’ang’ania kileleni na kila mchezo
inashinda na kuzidi kutupa wakati mgumu, kwa sababu hata Simba safari hii nao
wamejiandaa na wanashinda mfululizo, kwa hiyo hii inatupa wakati mgumu wa
kutwaa ubingwa.
“Tutakapokutana
nao, mechi haitakuwa nyepesi hata kidogo, wao wamejiandaa safari hii kama
wanavyoonekana lakini hata na sisi pia tumedhamiria kuchukua pointi tatu katika
kila mchezo, kwa hiyo tusubiri dakika 90,” alisema Sure Boy.
Yanga iliyo
kileleni mwa msimamo wa ligi inatarajia kuumana na Azam wanaoshikilia nafasi ya
pili Oktoba 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
0 COMMENTS:
Post a Comment