Kufuatia hali ya kukosa mikwaju ya penalti iliyowakumba wachezaji
wa Yanga, baadhi ya wachezaji wa timu hiyo, wametamka kuwa wanaweza wakaja
kugomea kupiga mikwaju hiyo pale watakapopata katika michezo yake ya ligi kuu,
kutokana na kuondokewa na kujiamini pale wanapoenda kuipiga.
Katika kipindi cha hivi karibuni kwenye michezo dhidi ya Toto na
Azam, licha ya kikosi hicho kupata mikwaju hiyo, wachezaji wake Thabani
Kamusoko na Donald Ngoma walijikuta wakiikosa na kuendeleza rekodi ya wachezaji
wa kikosi hicho kukosa mikwaju hiyo.
Awali, Yanga ilikosa mikwaju mingi ya penalti kwenye mechi za
Kombe la Kagame.
Mmoja wa wachezaji hao, Simon Msuva, alisema licha ya yeye
kuchaguliwa kupiga mikwaju hiyo inapotokea uwanjani, kwa sasa anaweza asipige
kutokana na kuondokewa na hali ya kujiamini pale anapokwenda kupiga,
inayochangiwa na wachezaji wengi wa kikosi hicho kukosa mikwaju hiyo.
“Unajua kuwa sasa yaani
wachezaji tuna hofu kubwa ya kupiga penalti kutokana na hali hii ya kuikosa
mikwaju hiyo pale inapojitokeza, jambo ambalo linatufanya kuendelea kuikosa
mikwaju hiyo kama ilivyotokea kwa Ngoma leo (wiki iliyopita) tulipocheza na
Toto.
“Lakini licha ya kuogopa mikwaju hiyo, naamini mwisho wa siku
tunaweza kuja na jawabu la kupiga mikwaju hiyo, kwani kila kitu kina mwanzo na
mwisho wake na naamini kocha tayari ameshaliona tatizo hili na atalifanyia
marekebisho,” alisema Msuva mwenye mabao matatu katika ligi.
Kwa sasa mikwaju hiyo ya Yanga inapigwa na wachezaji, Haruna
Niyonzima, Donald Ngoma pamoja na Msuva ikiwa ni baada ya kupewa jukumu hilo na
kocha wa kikosi hicho, Mholanzi Hans van Der Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment