Mashabiki wa timu ya taifa, Taifa Stars, bado wana taharuki ya
matokeo ya sare ya 2-2 dhidi ya Algeria lakini nahodha wa Stars, Nadir Haroub
‘Cannavaro’ ametamka kishujaa kuwa kazi bado haijaisha na anaamini timu hiyo
itafanya makubwa kutokana na safu kali ya ushambuliaji waliyonayo.
Stars ilicheza mpira mwingi katika mechi hiyo iliyopigwa juzi
Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar kwa ajili ya kufuzu kushiriki Kombe la
Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Cannavaro amesema kuwa mpira ni mchezo wa makosa na imetokea
bahati mbaya wametoka sare ya mabao kwenye uwanja wa nyumbani lakini bado
anaamini kuwa safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inayoongozwa na Mbwana Samatta
na Thomas Ulimwengu wanaokipiga TP Mazembe ya DR Congo, inaweza kufanya makubwa
katika mchezo wa marudiano kesho Jumanne nchini Algeria.
Samatta aliwafunga Waalgeria, USM Alger nyumbani kwao katika
mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika alipokuwa akiichezea TP Mazembe,
hivi karibuni.
“Bado mechi haijaisha, tumetoa sare hapa kitu ambacho si faida
sana kwetu lakini naamini kule kwao pia tunaweza kufanya lolote na hata
kuwafunga naamini itawezekana tu, naiamini sana safu ya ushambuliaji, najua
itafanya kitu,” alisema Cannavaro.
Beki wa kushoto wa Stars, Haji Mwinyi, aliongeza: “Tumefungwa
kimchezo, watu wanasema labda mabeki tumeyataka, lakini hapana, jamaa walitumia
makosa yetu ambayo hatukudhamiria, ndiyo maana wametufunga, lakini bado kuna
marudiano, tutajirekebisha na tutafanya vizuri.”
0 COMMENTS:
Post a Comment