Matokeo ya sare ya 2-2 kati ya Taifa Stas na Algeria yamewaumiza
vibaya wachezaji nyota wa Stars, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kiasi cha
kuhisi kuishiwa nguvu na kuwapa kazi ya ziada baadhi ya watu wa jopo la ufundi
la timu hiyo kuwatuliza.
Hayo yalijiri wakati wachezaji hao wakiwa kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliopigwa
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mara baada ya kutoka uwanjani, wachezaji hao wanaoichezea TP
Mazembe ya DR Congo, walionekana kunyong’onyea, kukosa nguvu na hata walipofika
vyumbani, waliishia kulala sakafuni, kitu walichokatazwa kukifanya na mmoja wa
viongozi wa benchi la ufundi kwa kuwa wanahatarisha afya zao.
Lakini wachezaji hao hawakuonekana kujali, hata walipotaka
kuinuliwa, walionekana wazito huku wakiwa hawaongei chochote, baadhi ya memba
wa Stars walijaribu kumvua viatu Ulimwengu na kumshawishi asiwaze kilichotokea
kwani yanaweza kuwa makubwa lakini hakukuwa na mwitikio wowote.
Baadaye wachezaji wa Stars walilazimika kutoka vyumbani na kwenda
kuzungumza na Makamu wa Rais, Samiah Suluhu aliyekuja kushuhudia mchezo huo,
lakini bado kina Samatta hawakunyanyuka. Ikabidi itumike nguvu ya ziada
kuwashawishi kuwa wasipokwenda inaweza kutafsiriwa vingine, ndipo waliporudiwa
na nguvu angalau na kujinyanyua na kutoka vyumbani humo.
Kuhusiana na hilo, Samatta alikiri kujisikia vibaya lakini zaidi
akasema hawana uhakika wa kufanya makubwa Algeria kwa kuwa wana mzigo mkubwa
ambao unaweza kufuta ndoto zao zote za kusonga mbele.
“Tumetoa sare katika hali ya mchezo, siwezi kusema mengi lakini
mchezo wa marudiano ni mgumu sana, si rahisi kwa kweli, tuna kazi kubwa na kila
mmoja anawafahamu Waarabu, sijui, tusubiri marudiano,” alisema Samatta ambaye alifunga
bao la pili katika mechi hiyo, la kwanza likifungwa na Elias Maguli wa Stand
United.
Stars pamoja na mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo,
walikuwa na matumaini makubwa ya kuifunga Algeria kutokana na mpira mwingi
uliopigwa uwanjani hapo lakini pia mabao mawili ya kuongoza yaliwatia jeuri
Watanzania kabla ya matokeo kubadilika baadaye.
Huo ulikuwa ni mchezo wa raundi ya pili wa kufuzu kushiriki Kombe
la Dunia 2018 nchini Urusi. Marudiano ni kesho Jumanne nchini Algeria.
0 COMMENTS:
Post a Comment