November 30, 2015


Na Saleh Ally
WIKI chache zilizopita, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliamua kutangaza kamati ya kuisaidia Taifa Stars ambayo ilikuwa inaongozwa na Farouk Baghouza.


Lengo lilikuwa ni kusaidia mchakato wa kwenda kupambana na Algeria kuwania kuingia katika makundi kuwania kucheza Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Russia.

Mwenyekiti wa kamati, Baghoza naye akaamua kuteua kamati ndogondogo kama vile, kama kamati ya uhamasishaji na kadhalika.

Nilikuwa sehemu ya kamati ya uhamasishaji nikiwa mwenyekiti na kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani na kuishangilia timu yetu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa inaanzia nyumbani.

Mara tu baada ya kuingia kwenye kamati, ukaanza mzozo ambao ulitokana na mjumbe aliyeteuliwa Shaffih Dauda kugoma uteuzi huo na badala yake akaendelea kuiponda TFF na kamati.

Msisitizo wake ulikuwa ni kwamba yeye hawezi kuingia kwa kuwa hakukuwa na njia ya mkato ya kuisaidia Taifa Stars! Mzozo huo ulifika mbali kidogo alipoanza kuzozana na Mahmoud Zubeiry na Maulid Kitenge ambao walifanya mahojiano kupitia kipindi cha Sports Head Quarter cha EFM Radio. Hii ilikuwa ni siku moja tu baada ya mimi kuwaomba waniache nikazungumze na Dauda kuhusiana na mambo mawili.
Moja kuhusu kamati, kwamba kamati yetu si ya kiufundi au kuchangisha fedha. Badala yake ilikuwa ni kuwahamasisha Watanzania kwenda uwanjani tu, hivyo haiusiani na njia ya mkato hivyo aungane nasi na kama anaona hatafanya hilo jambo la kiutaifa, basi akae kimya ili sisi tupigane, tukishindwa kuwashawishi watu, kutakuwa na sehemu ya kujifunza.

Kitenge na Zubeiry walishindwa kuvumilia baada ya kumsikia tena Dauda akiponda usiku huo kwenye kipindi cha michezo cha Clouds. Mimi kidogo nilishituka, kwa kuwa sikuona sababu ya Dauda kuiponda kamati wakati ule kwa kuwa sikumsikia akizungumzia suala la kukuza vijana wakati wa mechi dhidi ya Nigeria au Malawi.  Vijana wanakuzwa pale Tanzania inapokutana na Algeria tu? Au wote tuache timu ife peke yake halafu tuanze kukuza vijana? Mbona hakusema kabla ya mechi hii!

Pia nikawa najiuliza maswali, walioamini ndiyo wakati wa kukuza vijana kwa kuwa tunakutana na Algeria. Wamewahi kujiuliza tuna viwanja vingapi vinatosha kusaidia kukuza vijana? Sasa mbona hawakulilia ujenzi wa viwanja kwanza halafu tufuatie kukuza vijana?
Hata kama hakukuwa na kamati, bado angeweza kuzungumzia pia maana suala la vijana pia haliwezi kufanywa na kamati ambacho huwa ni kitu cha muda mfupi kwa ajili ya jambo fulani. Niliamua kuwa mchunguzi kwanza kwa kuwa wajumbe wa kamati yangu waliokuwa kimya kabisa ni mimi na Edo Kumwembe.
Baadaye niligundua kwa uchunguzi wangu, kwamba lengo lilikuwa ni kuanzisha mjadala ambao ungesaidia mambo mengine kabisa ambayo hayakuwa na faida kwa taifa kwa wakati huo. Wako waliniambia bila ya kamati, suala la kampeni kuita watu lingekabidhiwa kwa Clouds FC ambayo ingeweza kuingiza mamilioni ya fedha, hivyo haikumfurahisha Dauda, ndiyo maana akaamua kupambana. Sikuwaamini, kimyakimya, nikasema “sidhani kama Shaffih anaweza kufanya hivyo”. Lakini nikaamua kunyamaza, nikaendelea na uchunguzi wa taratibu ambao ulinifundisha mengi sana.

Nilijifunza kupitia hilo suala la kamati, lakini bado safari hii nikajifunza mengi baada ya kulazimisha kujilipia na kuongezewa kiasi cha fedha kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kusaidia kuwaeleza Watanzania nini kilikuwa kikiendelea kwenye kambi hiyo iliyokuwa jijini Johannesburg.

Moja, nimegundua Watanzania wengi wanawatumia wanamichezo kwa kuwapumbaza wakianzisha hoja kwa madai kwamba wanaipenda nchi, kumbe ni waongo na wazandiki wakubwa, badala yake wanaangalia maslahi yao ndiyo maana utaona walifurahia sana Taifa Stars kufungwa mabao 7-0, jambo ambalo ni usaliti wa wazi, ubinafsi wa hali ya juu na uzandiki mkubwa usioweza kuvumilika.

Wako wenye vita na TFF, walirudisha vita hiyo kwa Taifa Stars, walitaka ifeli ili wathibitishe ubovu wa uongozi wa TFF, jambo ambalo pia naliita usaliti mkubwa kwa nchi yetu. Ninaendelea kusisitiza kwamba wanafiki wamekuwa wengi kuliko zamani, hofu yangu kwamba mchezo wa soka umebakiza asilimia 10 za kuweza kuendelea kwa kuwa hata watetezi, nao wanaangalia maslahi yao badala ya maslahi ya taifa.

Nimepigania maisha ya mpira nchini kabla ya  Leodeger Tenga hajaingia madarakani. Rais wa TFF sasa, Malinzi amenikuta nikiendeleza vita hiyo ambayo haitaisha hadi niondoke duniani. Na ikifikia ninamkosoa, kamwe siwezi kukubali taifa langu kuanguka ili Malinzi aonekane amefeli. Akifanikiwa, itakuwa furaha kwangu, akifeli nitamueleza ukweli lakini si chuki ya maisha binafsi niingize na kuacha kuijali timu yangu ya taifa. Baadaye, nitaelezea kwa nini nina hofu ya uraia ya baadhi ya watu kutokana na namna wanavyoweza kuibeza Stars kwa kuwa tu hawakufaidika.

Lakini pia niligundua kuwa kamati inapokuwa haina fedha, bado wengi hawawezi kuwa watendaji. Wengi wangependa kila kitu kitangulize fedha mbele na suala la uzalendo, linakuwa ni hadithi tu.

Watu wengi walilazimika kutoa fedha zao za mifukoni, kama ambavyo Kamati ya Taifa Stars ilivyolipia ndege na kutoa nusu ya fedha za kambi kule Afrika Kusini ambayo ni mamilioni ya fedha.

Lakini ilionekana kuna wengine wana uwezo wa kufaidika na imekuwa ni jambo la kawaida. Baadaye nitakueleza kuhusiana na maofisa wa TFF ambao walifuja tu fedha na hawakuwa na sababu ya kufanya hivyo wakati sisi tunasumbuka kwa kutoa fedha za mifukoni kukamilisha mambo yaende sawa hasa katika uhamasishaji.

Kingine ambacho niligundua, kwamba wachezaji wa Taifa Stars wengi wao ni vijana na si wazee kama wengi wanavyoamini au kupiga kelele, eti tunataka vijana. Wastani wa umri wa kikosi ni miaka 23 na wakongwe hawazidi watano.

Lakini ni kikosi chenye wachezaji wengi wasiojitambua, wasioelewa nini nchi yao inataka au wananchi wanataka kuona nchi yao inafika wapi ikiwezekana wanaona Yanga, Simba na Azam FC ni kubwa kuliko timu ya taifa!

Niligundua wachezaji wengi wa Taifa Stars, bado hawajajua umuhimu wa kikosi hicho na ukubwa wake kwa hisia za ndani ya mioyo yao na sikutoka kwenye ubongo wao. Huenda kwa kuwa wamepita njia ya mkato kufika hapo, au wameingia kwa ulaini kutokana na ushindani kuwa duni, hivyo kila kitu kinakuwa lahisi kabisa kwao.

Nitakuelezea namna nilivyolazimika kuzuia ndege ya Fastjet tena kwa ugomvi mkubwa kwa dani 35 isiondoke kwenye Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Oliver Tambo jijini Johannesburg kwa kuwa wachezaji watano walichelewa kuingia ndani ya ndege tena kwa sababu za kipuuzi kabisa.

Achana na hiyo, nitakueleza namna wachezaji wa Stars walivyoshindwa kupumzika usiku kwa kulala mapema, badala yake wakaonyesha tabia za ajabu, za ‘uswahilini’ kwetu, hali iliyonipa hofu na kuanza kaumini safari yetu bado ni ndefu sana.

MAKALA haya, mwanzo yalianza kutoka katika gazeti la Championi. MUEDELEZO, SOMA SEHEMU YA PILI.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic