November 30, 2015


Na Saleh Ally
UTAONA katika sehemu ya kwanza na kuelezea mambo mengi ambayo niliyaona baada ya kuingia kwenye kamati ya Saidia Taifa Stars ishinde.


Nilikuwa Mwenyekiti wa kamati ndogo ya uhamasishaji. Kazi yake kubwa ilikuwa ni kuhamasisha watu kwa wingi kwenda Uwanja wa Taifa kuishangilia Taifa Stars ikipambana na timu ngumu na kigogo wa Afrika ambaye anajulikana duniani kote.

Jana nilieleza nitazungumzia mambo mengi, nikianzia hali ilivyokuwa katika kamati, wale waliojitoa katika kamati akiwemo Shaffih Dauda na kuanza kushambulia, uozo wa ndani ya TFF lakini nidhamu mbovu na aina ya wachezaji tulionao.

Kelele za kamati:
Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuingia katika kamati yoyote ile. Nilikubali baadaya kuchaguliwa na Mwenyekiti Farouk Baghoza, sikuona shida kwa ni suala la utaifa. Kuita watu kwa wingi kuishangilia Taifa Stars zaidi ililenga kuipa nguvu timu.

Inawezekana kabisa, TFF wangeweza kufurahia mapato zaidi. Lakini sikuwa na mgawo au motisha, badala yake niliangalia suala la kuunganisha Watanzania kwenda kuishangilia timu kwa nguvu zote.

Dauda aligoma kuingia kwenye kamati, kama nilivyooleza jana ikafikia Maulid Kitenge na Mahmoud Zubeiry kuamua kujibu mashambulizi kutokana na kuchoka kwa kuwa Dauda aliendelea kushambulia akidai kamati haina lolote. Kilichowauma wawili hao, kamati tuliyokuwepo haikuwa ya ufundi au kuchangisha fedha. Badala yake kuwahamasisha Watanzania waende kwa wingi uwanjani ikiwezekana kuwazomea sana Waalgeria na kuipa nguvu Taifa Stars.

Kwa kuwa nilikuwa mwenyekiti wa kamati, nilipinga Kitenge na Zubeiry kumshambulia Dauda kama alivyokuwa akifanya. Niliwashauri sisi tuonyeshe ni wakongwe kuliko yeye ambayo ni hali halisi. Nikawashauri tuangalie tunachotakiwa kufanya katika kamati yetu hiyo ndogo na si kulumbana.

Baada ya hapo sikuridhika, nilitaka kujua kipi hasa kinamfanya Dauda aanze kuhubiri kuhusu suala la vijana leo! Taifa Stars ina mechi siku 14 zijazo, halafu eti mtu anaanza kuhubiri ukuzaji wa vijana. Nilianza kuona kama miujiza, sikukubali kwamba alikuwa na nia nzuri ya kuitetea nchi, nilipata harufu ya maslahi binafsi, nikaamua kuingia ndani zaidi kutaka kujua.

Uchunguzi wangu uligundua mambo mengi sana, nitaanza na machache. Baadhi ya niliopita nikichunguza walinieleza haya. Moja, Clouds FM wamekuwa wakiingia mikataba ya kuzitangaza Taifa Stars, safari hii kwa kuwa kulikuwa na kamati ambayo ilikuwa ikiwashawishi watu wengi kujitolea kutangaza bure, hilo lilimuudhi Dauda kwa kuwa kimaslahi, anakuwa hafaidiki. Maana kuna suala la kamisheni kwake!

Sikuamini kwa kuwa namjua Dauda ni mzalendo. Lakini nikajiuliza, katika mechi ambazo Clouds FM ilifanya kazi ya kuitangaza mechi hiyo, mbona Dauda hakuzungumzia suala la vijana?

Nikajiuliza tena, hivi Dauda alitaka vijana wa Tanzania wakue ndani ya wiki mbili ili waichezee Taifa Stars dhidi ya Algeria? Maswali yakawa mengi, lakini kimyakimya nikasema; “Shaffih ni mtu mwema, hawezi kufanya mambo ya kipuuzi kama hayo.”

Tofauti nilifikiri Dauda angeweza kuamini kuona taifa letu lilikuwa vitani. Hadithi ya Algeria ni timu kubwa na ngumu kufungika, si jipya. Huenda limezungumzwa miaka nenda rudi na hata watoto wa shule ya msingi wanalijua. Vipi ndani ya wiki mbili kabla ya Stars kuivaa Algeria ndiyo iwe ishu kubwa?

Kama taifa linakwenda vitani, halafu raia mwema anawavunja nguvu wanajeshi wake, unaweza kuamini mtu huyu ana mapenzi na taifa lake? Nikajijibu kimyakimya: “Shaffih ni mtu mwelewa sana, huenda alighafirika tu, baadaye ataelewa.”

Nilijua kamati isingecheza, isingeshangilia lakini ilikuwa ikijitahidi kufanya kila linawezekana kupitia timu hiyo inayoonekana si nzuri kwa wengine ijaribu. Lakini imeshindikana.

Ajabu zaidi, kweli katika maendeleo ya soka sasa unaweza kuzungumza kamati na kuifanya mjadala badala ya kusema Taifa Stars inapaswa iungwe mkono vipi? Hivi ukisikia Mtanzania mwenzako anasema anafurahia kuona timu ya taifa imefungwa, unaweza vipi kupima uwezo wa ufikiri, uzalendo wake na moyo wa utaifa?

Niliamua kuachana na hayo, najua ni ya kupita na huenda nashauri wanaozungumzia ukuzwaji wa vijana, bora wakaangalia zaidi na kulipigania suala la viwanja bora ili tuwasaidie vijana.

Kikubwa niwapongeze kila walioacha kazi zao na kupambana kuhakikisha Taifa Stars inakuwa ina nguvu. Imefungwa 7-0, nimefungwa mimi, wewe na mzalendo yoyote, achana na wanaoamini kipato kinazidi utaifa.

Kamati yetu haikuwa na fedha, tulijichangisha kupitia bajeti tuliyojiwekea, hatukuifikia badala yake tukapita tukiwaomba watu watusaidie matangazo, stori, makala ilimradi kuwahamaisha tu Watanzania. Ahsante sana Waandishi, wahariri na viongozi wakuu wa vyombo vya habari mliojitolea, bila ya kuangalia maslahi kwanza.

Nikiachana na hilo, sasa naingia katika mambo kadhaa niliyoyaona ndani ya siku zaidi ya 10 nilizokuwa katika kamati.

Maofisa wengi wa TFF si watu wanaolenga kutaka kuendeleza mpira. Wengi ni wazandiki, waliolenga kujifaidisha, wanaotaka kushibisha matumbo yao na kamwe hawana nia ya kusaidia Taifa Stars kama watu wengi ambavyo wamekuwa wakifikiria. Nitakueleza kwa nini.

ENDELEA KUSOMA SEHEMU YA TATU.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic