Na
Saleh Ally
JANA
nilianza kuchambua namna nilivyogundua wachezaji wa Taifa namna ambavyo
hawakuwa na nidhamu kwa kiasi kikubwa katika kambi kama vile kuchelewa wakati
wa chakula, kupanda basin a hata kuchelewa kulala huku wakichati kupitia
mitandao ya Facebook, Instagram na Whatsapp.
Maana
yake hawakuwa wakipumzika, huku wakijua wataamkaa asubuhi na mapema kwa ajili
ya kifungua kinywa, pia kwenda mazoezini. Sasa watu gani hawa wanataka
kuchungwa kama ng’ombe ili waishi katika utaratibu sahihi. Tena wakiwa katika
kiwango cha timu ya taifa? Upuuzi kabisa.
Niliishia
pale walipokuwa wakisimuliana kuhusiana na akina Mbwana Samatta na Thomas
Ulimwengu ambao wanachezea TP Mazembe. Kwamba nidhamu yao, iliwavutia na
wengine walitamani kufanya hivyo.
Mimi
sikuwahi kuwaona Ulimwengu na Samatta wakifanya hivyo, ila wachezaji na baadhi
ya memba wa benchi la ufundi walisema kama saa ya chai ni 1:30 asubuhi, basi
wachezaji hao wa TP Mazembe wangekuwa eneo husika saa 1:20 asubuhi wakisubiri
kwa dakika 10 nzima, muda ukitimia wanaanza kazi ya kula. Hali kadhalika, hata
upandaji basi kwenda mazoezini au kwenye mechi, wangekuwa pale chini dakika 5
hadi 10 wakisubiri kuingia. Wakati wengine wangeingia baada ya muda wa kuondoka
kupita!
Sasa
wanasimuliana, wanakubali wanachofanya wenzao ni bora lakini kutumiza hawawezi.
Wachezaji
walipewa siku mbili za kufanya manunuzi. Siku ya tatu, Mudathir Yahaya
alimfuata kiongozi wa msafara, Msafiri Mgoyi akiomba akafanye shopping tena.
Akakataliwa, tena akiambiwa huo ni mzaha.
Siku
ya safari, tulitakiwa kuwa uwanja wa ndege saa saba. Lakini saa tano tuliondoka
hotelini, tukafika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo saa zima kabla
ya desk la Fastjet halijafunguliwa ili tuanze kukatiwa tiketi maalum kwa ajili
ya kuingia kwenye ndege.
Kwa
pamoja tulisubiri kwa saa zima, walipofungua tulipeleka ombi ili mtu mmoja
atuhudumie maana tulikuwa timu nzima, likakubaliwa lakini kijana yule wa
Kisauzi, alikuwa anafanya mambo yake taratibu.
Licha
ya kuwa nimeishapata tiketi yangu, mimi niliamua kubaki kati ya watu wa mwisho
kuhakikisha wenzangu wote wameingia na mwisho baada ya yule kijana wa shirika
la ndege kumaliza, nikaongozana na baadhi ya maofisa wa TFF, memba wa benchi la
ufundi moja kwa moja, kwenda kwenye ndege.
Ajabu!
Wakati tunaingia ndani ya ndege, kila abiria akiwa ameishaingia, wachezaji wa
Taifa Stars, hata walimu wao hawakuwa wameingia ndani ya ndege. Mmoja wa
maofisa wa TFF tuliokuwa tukisaidiana nao pale kwenye desk kuhakikisha
wachezaji na makocha wanakuwa wa kwanza kuingia, akadhani tumekosea ndege.
Kazi
ya kuanza kuwapigia simu ikaanza, dakika 10 baadaye walikuwa katika ndege.
Walidai walikuwa wanamalizia kula! Tiketi kawaida zinaandikwa muda wa kuingia
kwenye ndege, pia muda wa kuondoka, ninaamini wote wanajua kusoma namba!
Baada
ya kuona kazi imeisha, wakati maofisa wa Fastjet wanataka kufunga mlango,
ikagundulika abiria watano walikuwa hawajaingia ndani ya ndege! Wachezaji
waliokuwa ndani ya ndege wakasema John Bocco na Shomari Kapombe ndiyo walikuwa
hawajaingia, mbaya zaidi hawakuwa na simu zenye namba za Afrika Kusini na
wakati huo hawakuwa na ‘bando’ maana walitumia internet ya hotelini.
Maofisa
wa Fastjet walijitahidi kusubiri kwa dakika 15. Wakasema sasa ni muda wa
kuondoka kwa kuwa kuendelea kuchelewa, walikuwa wakilipa ushuru wa uwanja
zaidi.
Ukiwaacha
wachezaji hao itakuwaje? Tena wachezaji wamesema ameongezeka na Himid Mao, sasa
ni watatu. Dakika tano baadaye wakasema yumo na Aishi Manula.
Mimi
na ofisa mmoja wa TFF tulisimama na kusema ndege haitandoka, kama imeshindikana
washushe mizigo ya sisi sote.
Kwao angalau ikawa mtihani, tukaomba wamruhusu
Baraka Kizuguto ashuke kwenda kuwatafuta na mimi nina simu kwa namba ya Afrika
Kusini kama ilivyo kwake, ingekuwa lahisi kuwasiliana naye.
Zilishafika
dakika 20 na ushee, Kizuguto alipewa dakika 5 za kwenda kuwafuata, jamaa
walifanya hivyo huku wakijua walikuwa wakivunja kanuni za mambo ya anga.
Dakika
tano zilipita, Kizuguto hakuwa amerudi na wachezaji walikuwa hawajaonekana,
nilipompigia akasema hajawapata naye alikuwa njiani anarejea katika ndege.
Maofisa
wa Fastjet uvumilivu ulikuwa umewashinda na sasa walisema hata sisi kama
tunataka, basi tukashushe mizigo yetu tubaki kwao poa tu maana
‘tuliishawazingua’ vya kutosha.
Dakika
tano baadaye, tuliowana wachezaji hao wanakuja wakiwa wamebeba rundo la mifuko
baada ya kupiga shopping ya uhakika, tena hawakuwa wanne, walikuwa watano,
aliongezeka Mudathir ambaye watu walimsahau.
Ndani
ya ndege tayari kulikuwa na tafrani kati yangu na baadhi ya abiria wazungu
ambao walikuwa wakilaamini kucheleweshwa na walikuwa na haki. Tena walisisitiza
wachezaji wetu hawakuwa na nidhamu kwa kuwa hawajui hata kujali muda.
Wachezaji
wakati wanaingia ndani ya ndege walitoa sababu ya kijinga kabisa. Eti
walipotea, jambo ambalo lilikuwa haliwezekani kwani walikuwa wanaongozana
wakati wanaingia ndani ya ndege, vipi wengine wapotee wakati ni msafara wa watu
wengi?
Tena
kitu kibaya zaidi, wote watano walikuwa wanatokea klabu moja ya Azam FC ambalo
si jambo zuri kwa uongozi wa klabu.
Lazima
tukubali wachezaji wetu pia ni sehemu kubwa ya tatizo, kwamba kama wao
hawatabadilika hata taifa Stars ikipewa nini haitawezekana.
Tunataka
kukuza vijana, ndiyo ni jambo jema. Lakini kuwakuza bila kujadili misingi
sahihi na kutumia wataalamu wa uhakika ni kupoteza muda.
Wachezaji
wa Stars hasa waliokuwa wakifanya madudu, asilimia 90 ni hao wanaoonekana
makinda au vijana kwa kuwa wengi wana miaka 20 hadi 26. Sasa vijana, lakini si
wale waliokulia katika mazingira sahihi.
SOMA
SEHEMU YA SABA AMBAYO NDIYO YA MWISHO.
0 COMMENTS:
Post a Comment