November 30, 2015


Na Saleh Ally
JUZI Jumatano, nilielezea kuhusiana na wale viongozi rundo wa TFF waliosafiri na timu. Wengi hawakuwa nafaida yoyote ya safari hiyo badala yake walikwenda kama sehemu ya kwenda tu kwa kuwa kuna fedha za kuwaruhusu kwenda.


Huenda waliona kila kitu kinawezekana kwa kuwa kuna fedha za udhamini wa Kilimanjaro dola milioni 2, kwa mwaka zinazotolewa kwa ajili ya kuidhamini Taifa Stars.

Waliona inawezekana kwa kuwa tayari kamati ilijitokeza na kupunguza gharama ya mambo mengi ikiwemo kambi. Hivyo fedha ambazo zingeweza kutumika katika mambo mengine muhimu, wao wakaona zinaweza kutumiwa na wao kufurahia na kwenda kufanya ‘shopping’ ambalo lilikuwa ni jambo linaloonyesha wengi si wazalendo, hawako kwa ajili ya timu na wanaangalia zaidi maisha yao.

Ningependa kuzama zaidi hata aina ya mfumo wa utendaji wa TFF ambao unaonekana ni “one man show”. Mtu mmoja au kikundi Fulani kimejichukulia nguvu na kuwa sasa kinafanya kinachotaka hata kama watendaji au wahusika, hawana uwezo kitaalamu wala uzoefu.
Tuachane na TFF, huenda siku nyingine nikawa na nafasi ya kuzama zaidi kwa kina na kufunua madudu rundo ambayo ninayajua. Vema Watanzania wakajua maana kuna watu watano ambao uwezo wao ni ziro, lakini wanashikilia sehemu nyeti na kamwe kwa utendaji wao ulivyo, hakuna nafasi ya maendeleo hata kama watakuzwa vijana 1000!

Acha nitumbukie katika ile kambi ya Taifa Stars iliyokuwa pale Johannesburg nchini Afrika Kusini. Nilisema kambi ilikuwa katika hoteli bora ingawa haikuwa ya kifahari kupindukia. Lakini hakika wachezaji au benchi la ufundi, haliwezi kuwa na lawama.

Niwapongeze TFF na kamati kwa kambi hiyo. Lakini nikashangazwa kabisa na mienendo au maisha ya wachezaji ambao hakika ninaweza kukueleza nao ni tatizo kubwa.
Ninataka kubainisha matatizo haya, kama utakuwa una nafasi, hifadhi ili ujue tunakwama sehemu nyingi sana.

Wachezaji wengi wa Taifa Stars hawana nidhamu kabisa. Ninaposema hivyo, sina maana ile nidhamu ya kusema “shikamoo” au kuweka mikono nyuma wanapokuwa wanazungumza na mtu anayewazidi umri.

Nifafanue kwa kusema wengi si wachezaji wanaojitambua, hawajui kwa nini wako TAifa Stars na huenda hawajui kuwa timu hiyo ya taifa ni kubwa kuliko klabu wanazozichezea. Wapo tu kwa kuwa wapo na inaonyesha wanaamini kuwepo kwao pale wanaamini wanaisaidia TFF au wanawasaidia Watanzania.

Nilianza kushangazwa na tabia ya kuona wachezaji wengine wakiwa katika basi, halafu wengine wanasubiriwa hadi unapofikia muda wa kwenda mazoezini, wakati mwingine basi linalazimika kusubiri kwa kipindi fulani, eti fulani hajashuka katika basi.

Suala la kuchelewa liliendelea kujitokeza kadi katika chakula. Wengine wamefika na wengine wangefika nusu saa baadaye tena wakitembea kwa mwendo wa kujidai tu. Jambo ambalo lilionekana hawakuwa wakielewa maana hasa ya timu.

Ukiachana na hilo, niliona jambo jingine la ajabu kabisa! Nikalazimika kwenda kuzungumza na Charles Boniface Mkwasa ambaye alikiri kwamba aliliona na amelimekea mara kadhaa.

Wachezaji kuwa busy na Whatsapp, Instagram na Facebook. Wachezaji wengi wa Taifa Stars walikuwa si wachezaji wa soka, badala yake ni wacheza mitandao.

Wengi wao walipoteza muda mwingi wakisoma mitandao hiyo maarufu ya kijamii, tena wasivyo na haya hata kidogo walikaa kwenye korido ya hoteli hadi saa 7 usiku eti “wanachati”.

Nilishangazwa nilipowakuta Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Ibrahim Ajibu wakiwa wametoa mito chumbani mwao halafu wamelala pale korido kila mmoja karibu na chumbani kwake, “wanachati”.

Wanafanya hivyo wakiwa kifua wazi, wamevaa bukta tu. Ajabu wamesahau hiyo ni njia ya wapangaji wengine kwenda kwenye vyumba vyao, hivyo lazima waombe wakunje miguu au wawaruke ili kupita kwa kuwa pale walipolala, kichwa kinakuwa upande wa ukuta mmoja, miguu ukuta mwingine. Wameziba kabisa njia.

Jiulize TFF, kamati zimelipa fedha kwa ajili ya chumba chenye kitanda kizuri, mazingira bora. Lakini mchezaji anatoka nje na kwenda kulala kwenye njia tena akitumia mtu ambao baadaye ataurejesha kitandani na kulalia, huo ni uchafu na uswahili wa kupindukia.

Wachezaji haohao, ndio waliokuwa wakihadithiana kuhusiana na nidhamu ya juu ya Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu! Unajua walikuwa wanasemaje?

ENDELEA KUSOMA SEHEMU YA SITA


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic