RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI AKIWA NA RAIS WA CAF, ISSA HAYATOU (KATIKATI) PAMOJA NA RAIS MSTAAFU WA TFF, LEODEGER CHILLA TENGA. |
Na Saleh Ally
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) ndiyo linalopewa nafasi
kubwa kusimamia maendeleo ya soka nchini na lazima tukubali, ambayo yamekuwa
yakipigiwa kelele, huenda sasa yameanza kujiendesha.
TFF imekuwa ikilalamikiwa katika suala la
usimamizi wa mambo. Huenda wengi wakawa wamepata nafasi nyingi ya kupaza sauti
kwa sauti ya juu baada ya timu yetu ya taifa, Taifa Stars kufungwa mabao 7-0 na
Algeria.
Kipigo hicho, huenda kikawa mwanzo mpya ya
wale ambao hawakuwa wamewahi kusikilizwa kwa kile ambacho kimekuwa
kikizungumzwa na wadau wengi na huenda hakikupewa nafasi ya kusikilizwa au
kufanyiwa kazi.
Hivi karibuni, tumeona Rais wa Tanzania,
John Pombe Magufuli akifanya ziara za kushitukiza katika sehemu ambazo ni
taasisi za serikali.
Amefanya hivyo baada ya kugundua kumekuwa na
uzembe wa kupindukia. Kweli kila sehemu aliyokwenda mambo yameonekana kuwa
magumu na mwisho mabadiliko yamefanyika.
Baada ya ziara hizo za Magufuli, sehemu
nyingine ambazo ni ofisi za serikali, wameamka angalau hata kuanza kupanga
mafaili yao vizuri kwa kuwa wanajua Magufuli anaweza ‘akaibuka’ wakati wowote
na wenyewe wakaingia kwenye matatizo.
Hivyo wamerejea katika utendaji bora na
kuanza kuwatumikia wananchi katika kiwango sahihi kinachotakiwa. Hii ni sehemu
ya udhaifu mkubwa ya sisi Watanzania, kwamba ni watu tunaotaka kuchungwa kama
wanyama ili kufanya mambo yetu katika usahihi au ubora unaotakiwa.
Moja ya matatizo makubwa ndani ya shirikisho
hilo la soka nchini ni ushikaji au kupeana nafasi ndani yake kwa kupeana kwa
kuwa fulani ni mshikaji na anakuwa hana mashiko au faida hata kidogo katika
uendelezaji wa soka nchini.
TFF inaweza ikawa na watu wengi ndani,
lakini si wale ambao wana uwezo kwa ajili ya kusukuma maendeleo kwa kuwa uwezo
wao ni mdogo au hawana vigezo vya kukaa katika nafasi husika.
Mara kadhaa, nimekuwa nikipiga kelele
kuhusiana na mshauri wa ufundi wa Rais wa TFF. Kwamba ni mtu ambaye hana vigezo
na hawezi kuwa msaada kwa kuwa hana rekodi yoyote ya kufanya vizuri katika
chochote naye amekuwa akijisifia uwezo mkubwa wa fitna jambo ambalo, kamwe si
la ufundi.
Lakini bado TFF haina haja ya kumsubiri
Magufuli atue pale ili ianze kufanya mabadiliko. Badala yake sasa ndiyo wakati
mwafaka wa kufanya mambo bora na sahihi kipindi hiki.
Hakuna ujanja, huu ndiyo wakati wa Rais wa
TFF, Jamal Malinzi kuanza upya kuangalia katika vitengo vyake kuwa watu
aliowaweka katika vitengo vya ufundi, masoko, ushauri, uendelezaji vijana na
mambo mengine kama ni sahihi.
Wanapaswa kuwa watu sahihi ambao watasaidia
maendeleo ya mchezo wa soka nchini na wasiwe waliowekwa kwa kuwa tu wanaonyesha
mapenzi makubwa kwa Malinzi.
Kuonyesha mapenzi makubwa kwa Malinzi bila
ya kumkosoa ni uoga na unafiki au ninaweza kuuita kuficha uwezo mdogo na kama
utaendelea kuendekezwa ndiyo utakaokuwa ukiendelea kutumaliza na TFF itabaki
kama taasisi ya kuwafurahisha, kuwalipa fadhila na kuwatafutia watu riziki kwa
njia ya mkato.
Ofisa
Masoko anafiti katika nafasi yake? Kazi ya Matandika ni sahihi, kweli anahitajika
TFF, Baraka Kizuguto anafanya mambo yake kwa usahihi? Baada ya hapo, kuna haja
ya kuangalia wasiofaa waondolewe wapewe nafasi walio sahihi, pia wapewe nafasi
ya kutimiza majukumu yao kwa ufasaha.
Hakuna maendeleo yanayopatikana kwa utendaji
kazi huku yakiwa yamezungushiwa kivuli cha ushikaji. TFF ni taasisi ya umma na
hili wote waliopo pale TFF akiwemo Malinzi wanapaswa kulitambua.
Malinzi pia anapaswa kujua, washikaji
wamewaangusha watu wengi sana hasa viongozi na wafanyabiashara wakubwa. Hivyo hapaswi
kuhofia atakosa kura muhula unaofuata kama atakuwa amechapa kazi kwa uadilifu
na mafanikio yakaonekana. Ushikaji isiwe nguzo ya baadaye wakati maendeleo
hayapatikani.
0 COMMENTS:
Post a Comment