Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa
amewashukuru watanzania kwa kuwapa sapoti katika michezo miwili ya kuwania
kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa
mikutano wa TFF uliopo Karume, Mkwasa amesema pamoja na kupoteza nafasi ya
kusonga mbele katika hatua ya makundi kuwania kufuzu Kombe la Dunia nchini Russia mwaka 2018, anawashukuru Watanzania wote kwa ujumla kwa sapoti
waliyowapatia.
“Tumepotezea mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria,
wenzetu walituzidi kiufundi, uwezo wa wachezaji binafsi ulikua chachu ya kuweza
kuibuka na ushindi nyumbani kwao. Lakini bado Watanzania waishio Algeria na
washabiki waliokuja uwanjani walitusapoti katika mchezo huo kuanzia mwanzo hadi mwisho,” alisema Mkwasa.
“Tupo katika kipindi cha kujenga timu, tuna vijana
wengi wanaochipukia, hivyo wanahitaji muda wa kucheza zaidi na kupata uzoefu, tuendelee
kuwapa sapoti vijana hawa kwa ajili ya kujenga kikosi bora cha baadae”
ameongeza Mkwasa.
Mkwasa amewaomba watanzania kuendelea kuwasapoti
vijana, pamoja na matokeo mabaya dhidi ya Algeria, bado kuna nafasi ya kufanya
vizuri katika michezo inayofuata ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la
Mataifa Afrika mwaka 2017.
Naye, nahodha msaidizi wa Taifa Stars, John Bocco
ameishukuru TFF kwa kuwapatia huduma bora za maandalizi na wakati wa michezo
yao yote, amewashukru watanzania na vyombo vya habari kwa kuwapa sapoti na
kuwaomba kuendelea kuwaunga mkono pindi wanapokua na majukumu ya kuiwakilisha
nchi katika michuano mbalimbali.
“Matokeo ya juzi (dhidi ya Algeria) sisi wachezaji
yametusikitisha, tulikua na malengo na mtazamo tofauti wa kupata ushindi, lakini
katika mpira kuna matokeo matatu, tumepoteza mchezo huo kikubwa ni kujipanga
kwa ajili ya michezo ijayo na watanzania muendelea kutusapoti timu ya Taifa
kama ambavyo mmekua mkifanya kwa sasa,” alisema Bocco.
Stars imerejea leo alfajiri ikitokea nchini Algeria
ilipokua na mchezo wa marudiano dhidi ya Algeria, Jumanne katika uwanja wa
Mustapher Tchaker mjini Bilda ambapo ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 7
-0.
0 COMMENTS:
Post a Comment