Yanga ina washambuliaji watatu wa kutegemewa ambao ni Donald
Ngoma, Amissi Tambwe na Malimi Busungu, lakini bado haijatosheka, uongozi wa
timu hiyo upo kwenye mipango ya kusajili straika mwingine wa kazi.
Awali, mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, walitangaza kwamba
hawatasajili mchezaji yeyote wakati huu wa dirisha dogo lakini wametengua kauli
yao, baada ya kuona jinsi wapinzani wao Simba wanavyojiimarisha.
Straika huyo amepangwa kusajiliwa kwenye usajili wa dirisha dogo
msimu huu kwa ajili ya kuichezea timu hiyo kwenye Ligi Kuu Bara na Ligi ya
Mabingwa Afrika, mwakani.
Yanga inataka kusajili straika mwingine baada ya kocha mkuu wa
timu hiyo, Hans van Der Pluijm kupendekeza kutokana na Busungu kuhamishiwa pembeni
namba 11 iliyokuwa inachezwa na Andrey Coutinho na Geofrey Mwashiuya.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, alisema kuwa mshambuliaji
wanayemtaka ni yule aliye tayari kwa ajili ya kucheza ligi kuu na michuano mingine.
Dk Tiboroha alisema, straika huyo wanayemtaka ni yule atakayefanya
mazoezi na timu siku mbili na siku inayofuata anaingia uwanjani kwa ajili ya
kufanya kazi na siyo vingine.
Aliongeza kuwa, huo ndiyo mfumo wa usajili watakaoutumia katika
usajili wa wachezaji wao kimataifa katika kuhakikisha timu yao inakwenda
kisasa.
“Yapo mapendekezo mengi ya usajili yaliyotolewa kutoka katika
benchi letu la ufundi, moja kati ya nafasi tunayoitazama hivi sasa ni safu ya
ushambuliaji ambayo lazima tusajili.
“Hivyo kama usajili huo tutaufanya, basi lazima tumsajili straika
wa kazi mwenye uwezo wa kufunga mabao na aliye tayari kwa ajili ya kufanya kazi
na siyo kumfanyisha majaribio.
“Straika huyo tutakayemsajili ni yule atakayeendana na kasi kwa
maana ya kufanya mazoezi kwa siku mbili na kesho yake akaingia uwanjani kufanya
kazi kwa kucheza mechi na siyo kutoa muda wa majaribio,” alisema Dk Tiboroha.
0 COMMENTS:
Post a Comment