Na Saleh Ally
RAIS
John Joseph Pombe Magufuli amekuwa na sifa ya kutokuwa shabiki wa michezo lakini
mara kadhaa yeye amekuwa akieleza namna ambavyo amekuwa shabiki wa michezo
mbalimbali na aliwahi kuwa kipa.
Kila
binadamu ana haki ya kuchagua anachotaka, lakini linapofikia suala la majukumu,
sasa inakuwa ni uwajibikaji badala ya kufurahisha nafsi kutokana na
unachokihitaji.
Bado
sijawa na uhakika wa asilimia mia kwamba Magufuli ni shabiki wa mchezo gani, au
anaipenda michezo kwa kiasi kipi au kiwango kipi.
Ninaweza
kusema kwamba kwa mara ya kwanza ameanza na soka kwa kuonyesha anaipenda
michezo au anaithamini na kuipa heshima ya juu kama sehemu ya kipaumbele.
Magufuli
amekubali kuwa mgeni rasmi katika mechi ngumu ya kimataifa wakati Taifa Stars
itakuwa inakutana na Algeria ambao ni vinara au wababe wa Afrika kisoka.
Timu
ambayo michuano ya mwisho ya Kombe la Dunia iliyofanyika nchini Brazil, ilikuwa
kinara kwa timu za Afrika.
Timu
ambayo ni moja ya zile zilizoshiriki Kombe la Dunia mara nyingi ikitokea barani
Afrika. Stars inakwenda kukutana nayo, kupambana nayo na kulenga kuisimamisha.
Magufuli ameonyesha si mwoga kama baadhi ya viongozi ambao wamekuwa na hofu
kama timu ikifungwa, wao wako itaonekana kama hawakuwa wamesaidia.
Magufuli
anajua vijana wa Taifa Stars wanakwenda uwanjani kupambana na Algeria ambayo ni
sawa na vita ya Daudi na Goliath. Amekubali kuungana na watoto wake ambao ni
kina Daudi kwenda kupambana na mbabe huyo wa Afrika.
Magufuli
anaungana na Watanzania watakaokwenda uwanjani, kuwa sehemu ya wapambanaji
katika mechi hiyo ngumu kuliko zote ambayo Stars inakutana nayo mwaka huu.
Hata
ingekuwa Nigeria, Ghana au Ivory Coast wanakutana na Algeria. Lazima wachezaji
wao nyota kama Yaya Toure na wengine, wangelazimika kujiandaa maradufu kwa kuwa
wanajua mziki wanaokutana nao, hauchezeki kiulaini.
Magufuli
ametoa heshima kubwa sana kwa Taifa Stars, wapenda soka na wapenda michezo kwa
ujumla. Kazi itabaki kwao wachezaji, makocha wa timu pamoja na Watanzania
wenyewe wanaokwenda uwanjani Jumamosi kuishangilia timu kwa nguvu ili Rais
Magufuli aone yuko na watu sahihi na kweli alistahili kuungana nao kupambana.
Kamati
ya Taifa Stars ambayo imeshiriki kufanikisha au kuomba Rais Magufuli kujitokeza
inastahili pongezi. Kuweza angalau kujaribu na kusahau yaliyokuwa yakisemwa
kwamba Magufuli si mwanamichezo ni jambo la kupongeza.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Stars, Farouk Baghoza, Katibu, Teddy Mapunda na wajumbe wengine
wamekuwa wakipambana na ndiyo maana unaona maandalizi yamekuwa ya kiwango cha
juu. Vema wakaendelea kupambana hadi mwisho.
Kwa
Watanzania wengine, ushindi wa Taifa Stars utakuwa ni wa wote. Hakuna ujanja
sasa, itikadi za timu kwa maana ya klabu au vyama vya kisiasa ziwekwe kando na
pamoja tuungane kesho kuisaidia timu yetu.
Kila
mmoja anajua Stars itakapokuwa uwanjani Novemba 17, wenyeji raia wa Algeria wataizomea
ile mbaya kuhakikisha wanaichanganya ili kikosi chao kifanye vema.
Watafanya
hivyo kwa kuwa watakuwa wanalipigania taifa lao lifanye vizuri. Nafasi ya
Watanzania itakuwa ni kesho Jumamosi na vema kama wataitumia kwa kuwa Waalgeria
wao hawatafanya mzaha hata kidogo hiyo Novemba 17.
Kama ni Mtanzania, unabaki kuwa Mtanzania na
moyo wako utakuwa hapa Tanzania. Huu si wakati wa kulumbana na kusema hatuwezi
kabla hatujapambana. Twende tukapambane kwanza.
Angalia
rais wa nchi yetu naye anakuwa pale, vipi wewe uone haiwezekani au itakuwa
vigumu. Umetoa mchango gani au ushauri upi hadi kufikia kesho? Bado una nafasi
ya kulipigania taifa lako. Taifa Stars ni yako, yangu na ya wote.
0 COMMENTS:
Post a Comment