Huku pazia la usajili wa dirisha dogo Tanzania Bara likitarajiwa kufunguliwa
Jumapili ya wiki hii, uongozi wa Klabu ya Yanga umetamka kuwa hautafanya
usajili wowote ule mpaka uhakikishe unawauza baadhi ya wachezaji wake.
Yanga
ambayo ilianza mazoezi wiki hii baada ya mapumziko ya muda, inashika nafasi ya
pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 23, mbili nyuma ya vinara Azam FC.
Mkuu wa
Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, amesema wamepania
kufanya hivyo kwa kufuata ripoti ya kocha wa kikosi hicho aliyopendekeza
kutosajiliwa mchezaji yeyote mpaka pale watakapohakikisha wanauza baadhi ya
wachezaji.
“Licha ya
dirisha dogo la usajili ndiyo linataka kufunguliwa lakini kwa upande wetu bado
hatuna mawazo ya kusajili wachezaji wengine kutokana na hawa waliopo kocha
kupendekeza kuendelea nao wote katika michezo ijayo.
“Pale
tutakapohitaji kufanya usajili ni lazima tuhakikishe tunawauza wachezaji
waliopo ambao wanatakiwa na timu nyingine kwa ajili ya kukusanya fedha za
kununua wachezaji bora zaidi ya watakaokuwa wanaondoka ndani ya timu yetu,”
alisema Muro.
0 COMMENTS:
Post a Comment