MECHI ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga dhidi ya Mbeya City hakika ilikuwa tamu sana kwa maana ya uchezaji na ushindani.
Kila timu ilionekana imepania kushinda, kila upande ulicheza kwa juhudi na soka kwa maana ya pasi na mbinu, lilikuwa poa sana.
Uchezaji wa kiushindani, maana yake ni kuutafuta ubora. Yanga walionekana kuwa zaidi ya Mbeya City ambao katika mashambulizi hawakuwa wakali sana au hawakuwa na mipango bora zaidi kuhakikisha wanapata mabao.
Wakati wanapambana, kawaida mchezo wa soka unahusisha watu wanaoshinda, mara kadhaa hutokea mizozo na mambo ya ajabu.
Beki wa Mbeya City, Tumba Sued alimtandika ngumi au kofi mshambuliaji Donald Ngoma wa Yanga. Mwamuzi Jonesia Rukyaa kutoka Kagera akaliona na mara moja kulifanyia kazi.
Mwamuzi huyo mwanamama alitoa kadi nyekundu kwa Tumba kutokana na mchezo wake huo ambao haukuwa wa kiungwana.
Utaona wakati Tumba anampiga Ngoma, tayari mpira ulikuwa umeondoka katika eneo la tukio. Jambo ambalo unaweza kusema kwamba beki huyo ambaye ndiyo alikuwa anaichezea Mbeya City mechi yake ya kwanza akitokea Coastal Union, hakuwa makini na hakujitambua.
Mbeya City imemnunua Tumba kwa ajili ya kuisaidia safu yake ya ulinzi baada ya nahodha wake, Juma Nyosso kufungiwa kutokana na kuonyesha vitendo ambavyo havikuwa vya kiungwana uwanjani. Sasa Tumba naye ambaye amechukuliwa kusaidia, anarudi kulekule!
Lakini wakati mwamuzi huyohuyo akimtoa Tumba, akashindwa kufanya hivyo kwa beki wa Yanga, Vincent Bossou ambaye alimpiga mshambuliaji wa Mbeya City, Themi Felix tena wazi kila mtu akiona.
Tukio la Tumba na Ngoma, lilitokea karibu na mwamuzi na hakukuwa na tofauti na tukio la pili ambalo lilianza na tafrani ya Haruna Moshi ‘Boban’ wa Mbeya City kuanza kuzozana na Kelvin Yondani wa Yanga kabla ya wengine kuingilia.
Wakati wa masuala ya kuamua, Bossou raia wa Togo akampiga usoni Themi tena inaonekana wazi. Kafanya hivyo karibu kabisa na mwamuzi.
Huenda mwamuzi hakuona, lakini tukio lilitokea upande ambako anakuwepo mwamuzi msaidizi namba moja ambaye pia kama hakuona, kwa kuwa kulikuwa na tafrani, basi mwamuzi wa akiba pia hakuwa mbali sana.
Waamuzi watatu wanashindwa kuona tukio ambalo linatokea katika kipindi macho ya watu wengi yameelekezwa katika eneo hilo moja, kwangu naona kuna tatizo na kama itaendelea hivi; zitakuwa hisia na baadaye zitasababisha mfarakano mkubwa.
Tayari kuna taarifa za kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaipendelea Yanga, inawezekana hilo halipo, lakini hali inavyokwenda itafikia ikawa vigumu kubadilisha hisia au mawazo ya watu kwa kuwa kila kitu kinaendana na hali halisi.
Mwamuzi mmoja, anaweza kuona tukio moja, waamuzi watatu hawawezi kuona tukio moja! Lakini usisahau kwamba bado kuna kesi ya Ngoma kumpiga ngumi kwa makusudi beki Hassan Kessy wa Simba.
Waamuzi pia hawakuona, lakini TFF ambayo ilifikishiwa mashitaka nayo hadi sasa haijalifanyia kazi na sasa jambo hilo linaanza kuonekana ni kama “Mavi ya kale…..”
Lazima tukubali waamuzi pia mnakuwa sehemu ya tatizo na mnapaswa kuwa makini zaidi na kuachana na kulifanya suala la ubinadamu kama kigezo kikuu wakati huku makosa yanaonekana, kule hayaonekani.
Kuna kila sababu ya waamuzi kuanza kuona ufanisi bora unatokana na ubora wa utekelezaji kwa usahihi kwa wakati mwafaka na si maneno au visingizio.
Ili kuwe na ligi bora na bingwa halali, lazima haki iwe mwongozo na wahusika wakiwemo waamuzi, wachezaji, makocha na viongozi, wapite katika njia sahihi inayoongozwa na haki.
Mmh kaka na Bosou uliyekuwa unamponda ameanza kukudhuru!? Yanga amecheza game mbili wenzake wakiwa wamepumzika bado mnasema anapendelewa!? Hata ulaya si kila kosa huwa linaonekana na mtu aliyeshindwa kulalamika ni kawaida!!
ReplyDeleteUnatumiwa wewe!
ReplyDeleteTatizo la mkamata kalamu Saleh ni unazi wake kwa simba ndio sababu inayomfanya aonekane hafai kiuandishi.Acha mahaba katika kusimamia ukweli kwani visenti unavyopewa na hao wanaokusapoti wala havikupeleki kokote.Angalia lile tatizo la zungu wa simba na mangi wa yanga jinsi Saleh alivyolikuza,wakati waandishi wenzake wakiwa fair.acha kutumiwa dogo hapa ni bongo mambo yanaenda kibongobongo,hata hivyo ukitaka maisha murua basi pensa Yanga hao wengine ni magumashi tuu!
ReplyDelete