December 21, 2015



Na Saleh Ally
NILIMUONA Msemaji wa Yanga, Jerry Muro akivurumisha maneno ya kijinga kabisa kwa Msemaji wa Simba, Haji Manara aliyezaliwa Kariakoo, Dar es Salaam, nyumbani kwao kabila la Wazaramo, sikuamini!

Ulikuwa mkutano wa waandishi wa habari waliokuwa wamealikwa klabu Yanga. Najua walioinua mguu kwenye makao makuu ya Yanga pale Jangwani na Twiga walikuwa wanajua “Yanga inazungumza”.

Lakini mazungumzo niliyoyaona kwenye kipande cha picha ya video, kinaonyesha Muro akijielezea yeye namna alivyosoma nje ya Tanzania, anaendesha gari zuri na anaishi Mbezi Beach.

Kama haitoshi alifikia kusema kwamba yeye ni Mchaga, amekuja mjini kutafuta fedha na si kuendekeza maneno, halafu akasisitiza mara mbili yeye si Mzaramo!

Wakati Muro akizungumza hayo, alikuwa akimlenga msemaji wa Simba, Manara ambaye alilalama kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inaipendelea Yanga, iliamua kupitisha wachezaji waliosajiliwa na mambo yao kukamilika watumike. 

Manara alisema TFF ilifanya hivyo baada ya kuona Yanga imemsajili kiungo Issofou Boubacar kutoka Algeria. Lakini iliwazuia akina Paul Kiongera na Brian Majwega wa Simba kwa makusudi kabisa.

Muro hakujibu hoja hiyo ya Manara, lakini alikuwa akijibu hoja ambayo hakika ilikuwa haimhusu. Kiungwana angeweza kuendelea na mambo mengine ambayo ninaamini yalikuwa mahsusi.

Lakini pia nilishangazwa na waandishi waliokuwa wametulia wakimsikiliza Muro akijisifia kuendesha gari zuri (sijui la aina gani), kujisifia kuishi Mbezi Beach (akiwa amesahau mashabiki wa Yanga wako nchi nzima), tena akiwa amesahau hata makao makuu ya Yanga na ndiyo iliyomuajiri iko Kariakoo.

Kariako ni uswahilini na ndiyo chimbuko la Watanzania wengi. Mimi natokea uswahilini na hakuna anayeweza kubisha huko ndiko mpira unapochezwa. Hivyo Muro alipaswa kujua kama anaishi Mbezi Beach basi ni kwa ajili ya Yanga ambayo ipo Kariakoo, angepaheshimu na si kusema yeye haishi Kariakoo, anaishi huko anakoamini ni uzunguni.

Wakati natazama video hiyo, nilifikiria mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na kumtafuta Muro kama mshikaji na kumueleza madudu yake. Lakini naamini hii ndiyo njia sahihi kwa kuwa wakati anapovurugwa huwa ninamtetea, lakini kwa hilo alilofanya niseme ni upuuzi kabisa.

Ninaamini Yanga inapowaita waandishi kitu muhimu huwa ni masuala ya klabu na si hoja binafsi za wafanyakazi wake wanaotaka kujitangaza au kuwakashifu watu.

Nimeambiwa Muro amelalamika kwamba Manara alimtukana yeye pia. Lakini wapi? Hata ikiwa kweli, ilikuwa kwenye mkutano rasmi kama huo?
Iko haja ajifunze kwamba anapokuwa anazungumza mbele ya waandishi ni kwa niaba ya Yanga na si yeye tu au familia yake. Ikiwezekana ana kazi ya kuonyesha ubora wa elimu aliyoipata huko katika nchi mbalimbali, maana njia anayopita si sahihi na waandishi pia hawapaswi kwenda kumsikiliza yeye akijigamba binafsi badala ya kueleza Yanga ina kipi.

Wanachama wa Yanga wanapaswa kujua mambo mengi ya klabu hiyo ambayo bado yana maswali, huenda ni vizuri akipata nafasi kuyazungumzia.
Wakati mwingine najiuliza, kuwa hata taarifa kwa vyombo vya habari siku hizi imekuwa ni shida. Wasemaji wakipata nafasi wanabwabwaja madudu ambayo hayana msingi.

Niliona mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji wa Yanga, Mohammed Bhinda akiwaomba radhi Wazaramo kwa niaba ya Muro, jambo ambalo ni uungwana lakini bado si sahihi. Yanga imezaliwa Dar es Salaam, mkoa ambao Wazaramo ndiyo wenyeji. Hivyo wanahitaji heshima yao.

Viongozi wengi wa Yanga ni Wazaramo au watu wanaowaheshimu watu wa kabila hilo. Wako Wazaramo ni waasisi wa Yanga. Hakika Muro unapaswa kuchunga mdomo wako na ujue wakati wa kuzungumza na unasema kipi.

Binadamu wanakosea, lakini suala la kuomba radhi ni uungwana. Yale ya kwenye kamati ya maadili ulikoshitakiwa ni yako, lakini bado unatakiwa kuinua mdomo wako na kuwaomba radhi Wazaramo kuonyesha wewe ni muungwana.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic