Namna mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma kuzidi kuonyesha kiwango kizuri siku hadi siku na kuwa gumzo kila kona ya Bongo, sifa zake zimevuka mipaka hadi nchini kwao na kusababisha msafara wa watu tisa kuja kumshuhudia akifanya vitu vyake uwanjani.
Msafara huo wa Wazimbabwe tisa wake kwa waume ulikuwepo kwenye mchezo kati ya Yanga na Stand United uliopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa Dar ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0.
Ngoma ambaye mpaka sasa ameshaifungia Yanga mabao nane kwenye ligi, alikuwepo kwenye mchezo huo na kucheza kwa dakika zote 90 licha ya kutofunga bao hata moja lakini alitoa pasi ya bao lililofungwa na Amissi Tambwe.
Wazimbabwe hao walisema kuwa wamekuwa wakizisikia taarifa za Ngoma wakiwa kwao Zimbabwe ndipo wakaamua kuja kumshuhudia ‘live’.
“Nyumbani Zimbabwe zimetapakaa taarifa za Ngoma kuwa anafanya makubwa huku Tanzania, hivyo kila mtu ana hamu ya kumshuhudia, kwa kuwa tumekuja Tanzania kwa ajili ya ziara ya kimasomo pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) tukaona tuitumie fursa hiyo ili tumuone turidhike.
“Tukaongea na Jonas Tiboroha (Katibu wa Yanga) ambaye ni mwalimu pale chuo kikuu na akatuleta, bahati nzuri amecheza na kikubwa zaidi Mzimbabwe mwingine Thabani Kamusoko amefunga bao, tumefurahi kwa kweli kumuona Ngoma akicheza pamoja na Kamusoko kufunga bao,” alisema mmoja wao.







0 COMMENTS:
Post a Comment