Na Saleh Ally
WATANZANIA ni watu
wasiopenda kuambiwa ukweli hata kidogo, ni watu wanaofurahia kufanya maovu na
kukosolewa kwao linakuwa ni tusi.
Angalia Rais John
Magufuli na Serikali yake, wanachokifanya katika kipindi hiki kinaonekana ni
kitu kipya kabisa katika ulimwengu wa Watanzania.
Kinakuwa kipya kwa
kuwa wengi walifanya mambo kwa ujanjaujanja na upigaji, waliamini kuiba mali ya
umma ni haki yao na kitu kibaya zaidi walijijengea wigo, kwamba hakuna wa
kuwafanya kitu.
Unaona kiongozi
yuko ndani ya TFF, amepewa nafasi ambayo kiuwezo haiwezi na hawezi kuleta
matunda, lakini anafurahia kwa kuwa atapata fedha za kuendesha maisha yake.
Angalia ndani ya
klabu za Simba na Yanga, viongozi kibao tunawajua, wamediriki kugombea nafasi
za uongozi huku wakijua ndani ya nafsi zao kwamba hawana uwezo wa kuongoza
Simba.
Viongozi
wanaokwenda kugombea Simba au Yanga, hawakuwahi kuongoza hata timu ya mtaa.
Hawakuwahi hata kuona namna gani ai kipi kifanyike kusaidia maendeleo ya mpira.
Angalau wangekuwa
wamejifunza, angalau wangekuwa wana elimu ya kitu wanachotaka kukiongoza.
Pamoja na kujua hawana, lakini wanaamua kuingia kugombea, wakijua watapita njia
za mkato na kushinda ili waiongoze klabu.
Kama unakwenda
kwenye klabu, Yanga, Simba, Mtibwa Sugar, Azam FC na nyinginezo, unakutaka
viongozi wasio sahihi katika uongozi. Halafu unarudi kwenye ngazi ya
shirikisho, nako unakuta viongozi wasio sahihi na wasio na malengo ya
kuendeleza mchezo wa soka. Unategemea utaendelea vipi?
Asilimia kubwa ya
viongozi wa soka huona wanadhalilishwa pale wanaopoambiwa uwezo wao ni mdogo,
hakika wanakuwa wanajua wazi kwamba hawana uwezo wa kuisaidia au kuyasaidia
maendeleo ya soka hapa nchini.
Viongozi wa soka,
wengi wao ni wale wanaoingia katika nafasi nyingi, kwa kuwa tu wana uwezo wa
kuweka visingizo, kuanzisha kesi au kufanya chochote kuonyesha wamesingiziwa au
kuonewa hasa wanapoelezwa ukweli.
Katika upande wa
soka, malalamiko ya maendeleo kuwa duni ni makubwa sana. Viongozi wetu si watu
waaminifu na wanaotaka kujifaidisha wao wenyewe. Utaona walivyokuwa wamelala
viongozi wa sehemu nyeti nchini kama TRA, Bandari na kwingineko, mambo
yakasababisha hasara kwa Watanzania.
Ndivyo ilivyo
katika sekta nyeti za soka na michezo mingine. Wengi ni wapigaji, wenye maslahi
zaidi na maisha yao na si maisha ya soka na michezo kwa ujumla na kamwe
hawataki kuguswa kwa kuwa wanatengeneza uzio wasifikiwe au kuwekwa wazi.
Sidhani kama wadau
wa soka wanapaswa kumsubiri Magufuli aje kuondoa uozo huo. Badala yake wale
ambao wanajua uwezo wao ni mdogo, huu sasa ndiyo wakati mwafaka wa kuanza
kujiondoa taratibu na kupicha nafasi kwa wengine wenye uchungu na lengo la
kuendelea.
Kwangu ninaamini
huu si wakati wa kuogopa au kuwahofia watu tena. Si wakati wa kuhofia wanaotaka
kupunguza kasi ya kusema ukweli kwa vitisho vya kwenda mahakamani, vitisho vya
kuwamaliza watu kwa kuondoa roho zao.
Mchezo wa soka na
michezo mingine iko hatarini kuporomoka zaidi ya hapa kwa kuwa haina watu
sahihi. Huu ni wakati mwafaka wa kuwafichua na kueleza matendo yao, kukumbusha
maovu yao na kusisitiza kwa kuwataja kwa majina, kwamba wanapaswa kuondoka ili
wawapishe wengine waongoze soka na kuleta maendeleo.
Kiongozi
anakasirishwa kabisa kuambiwa hana uwezo, anaamini amedhalilishwa kwa sababu
kaelezwa ukweli. Lakini hana chochote cha mafanikio alichokifanya zaidi ya
kutumia vibaya fedha za Watanzania zinazopatikana kupitia soka.
Mimi nafunga uoga
huo, nitasimama hadi nitakapobaki peke yangu. Lakini nitakuwa niliyesema
ukweli, niliyepigania maendeleo ya michezo ambayo inayumba.
Ila safari hii
nitakuwa wazi zaidi, ikiwezekana kumzungumzia kiongozi mmoja zaidi ya mara moja
na kuweka wazi madudu yake bila ya woga wala kuogopa chochote.
Mlio katika klabu
za Simba, Yanga na nyingine, kumbukeni ni mali ya wananchi. Mlio TFF, msianze
kuamini ni mali yenu, misifikiri madudu mengi mnayofanya ni siri kubwa. Mimi
sitamsubiri Magufuli afike kwenu, nitapambana hadi mwisho na msitegemee uoga
kunizimbele ya uso wangu. Mnaweza kuchagua, mbaki na kuwa watendaji wa kweli,
au ondokeni muwapishe wenye uwezo wa kuusaidia mpira wetu.
Angalia leo, kila
sehemu tunakwama. Angalia hata katika viwango tu vya Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa), Tanzania inazidiwa na karibu kila nchi ya ukanda wa Afrika
Mashariki na Kati. Halafu, mnajisikia vibaya kuitwa mna uwezo mdogo!
0 COMMENTS:
Post a Comment