MZEE DALALI AKIWA KWENYE UWANJA WA NANGWANDA MJINI MTWARA, LEO. |
Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, amelaani kwa kiasi kikubwa vurugu walizofanyiwa wachezaji na makocha wa Simba mjini Mtwara.
Dalali maarufu kama Fiel Marshal amezungumza na SALEHJEMBE kutoka mjini Mtwara na kusema kwake ameona ni maajabu ya karne kwa vurugu na dharau kubwa walizofanya mashabiki hao wa Ndanda.
Taarifa nyingine zimesema Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, limewakamata na kuwatia mbaroni watu watatu ikiwa ni kati ya wale waliokuwa wakiwafanyia Simba vurugu.
“Niko hapa Mtwara, kwa kweli hali ilikuwa mbaya sana, hawa watu hawakuwa wastaarabu hata kidogo. Wamefanya mambo ya ajabu mimi sijaona katika kipindi changu chote cha uongozi wa soka.
“Wameingia uwanjani na kuwatukana sana wachezaji, wametukana matusi ya nguoni lakini niwapongeze wachezaji walivumilia sana.
“Walishuka hadi kwenye benchi la Simba pale, wakatukana sana, wakahamia jukwaani nako wakatukana sana.
“Hiyo haikutosha, wakati tunatoka wakaanza kutushambulia kwa mawe, sasa uzalendo ukawashinda vijana. Wakashuka na kuwakimbiza, wakawashika watatu na kuwazuia hadi Polisi walipofika pale, wakawaweka kizuizini.
“Kabla ya hapo, wachezaji walilazimika kusubiri saa zima ili kuingia kwenye uwanja kwa ajili ya mazoezi. Uongozi wa uwanja ulikuwa unazungusha na wale mashabiki walikuwa pale wakisema wazi kwamba hatutafanya mazoezi hapo kwa kuwa wameweka mambo yao ambayo sijui ni yapi,” alisema Dalali.
“Kweli hali haikuwa nzuri, mambo yalikuwa mabaya sana na washukuru mashabiki wa Simba kutoka Dar es Salaam hawakuwa wamefika. Ingekuwa maafa kwa kweli, tumshukuru sana Mungu.
“Lakini vipi watu wafanye Simba kama iko nchi jirani, nafikiri wanapaswa kuadhibiwa na kama ni sheria hakika ichukue mkondo wake,” alisema Dalali akionyesha kuchukizwa na jambo hilo.
Kali hali isiyokuwa ya kawaida, wachezaji wa Simba walijikuta katika wakati mgumu baada ya kuvamiwa na mashabiki wa Ndanda wakati wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Nangwana Sijaona mjini Mtwara, jioni hii.
0 COMMENTS:
Post a Comment