Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr amekiri kwamba uzembe ndiyo uliowakosesha ushindi katika mechi yao dhidi ya Toto African jijini Mwanza, jana.
Lakini akaongeza ubovu wa uwanja, ulichangia kwa kiasi kikubwa wao kushindwa kucheza soka safi. Katika mechi hiyo, Simba ililazimishwa sare ya bao 1-1 katika dakika za mwisho kabisa.
Akizungumza na SALEHJEMBE, Kerr amesema walikuwa na nafasi kubwa ya kushinda kwa kuwa waliwakamata Toto watakavyo.
“Uliona, tulijitahidi kuwadhibiti na kutawala mchezo, uwanja ulikuwa tatizo katika sehemu kubwa ya mechi hiyo.
“Ilikuwa vigumu kucheza mpira sahihi kama tulivyopanga. Lakini bado tulikuwa na nafasi ya kuibuka na ushindi kama tungekuwa makini.
“Mabeki wetu walishindwa kuwa makini hasa dakika za mwisho na wanajua tunatakiwa kufanya nini. Bado tuna nafasi ya kupambana, hivyo tunarekebisha makosa yetu.
“Kawaida unapofanya makosa katika ulinzi, basi watu wanakuadhibu.”
Baada ya kuibana Toto kwa dakika zote, Simba iliruhusu bao la dakika za nyongeza baada ya beki Isihaka Hassan kushindwa kuruka juu na kuuwahi mpira uliomfikia mshambuliaji wa Toto, akafunga kwa ulaini kabisa.








0 COMMENTS:
Post a Comment