![]() |
| MALINZI AKIWA NA RAIS WA CAF, ISSA HAYATOU |
Na Saleh Ally
UFALME wa Sepp Blatter katika uongozi wa soka duniani umesitishwa kwa kifungo cha miaka minane kutoka kwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Blatter alichukua urais wa Fifa mwaka 1998 ikiwa ni miaka sita tu baada ya Mbwana Samatta kuzaliwa, maana yake hakuwa ameanza hata darasa la kwanza.
Ameendelea kubaki kwenye uongozi hadi Samatta akiwa na umri wa miaka 23 na sasa ni staa Tanzania, DR Congo na Afrika nzima na anawaniwa na timu za Ulaya kutokana na ubora wake.
Kitu kizuri ni kwamba, mwisho wa Blatter umekuwa ni mbaya kabisa kutokana na kuondoka kwa kufungiwa kujishughulisha na masuala ya soka kwa miaka nane.
Blatter amefungiwa na Kamati ya Maadili ya Fifa kujishughulisha na soka kwa miaka nane baada ya kupatikana na hatia ya kuidhinisha kimagumashi dola milioni 2 (Sh bilioni 4) kwa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Fifa, Michel Platini ambaye pia amekumbana na adhabu kama hiyo kwa kuwa ndiye aliyepokea fedha hizo kama malipo ya kuwa mshauri wa Blatter.
Rais huyo aliyekuwa kama mfalme wa Fifa, amehukumiwa miaka minane katika kifungo cha soka kupitia kamati ya maadili ambayo aliiteua.
![]() |
| BLATTER |
Kamati ya Maadili ya Fifa yenye wanasheria wanne, ilifikia uamuzi huo baada ya kumpa Blatter nafasi ya kujitetea kwa saa nane mfululizo. Mwenzake Platini yeye alikaidi na kuamua kutoa maelezo yake kwa maandishi kupitia mwanasheria wake aliyejitokeza mbele ya kamati.
Kamati aliyoiteua Blatter, leo ndiyo imefanya kazi ya kumfungia kwa ubadhirifu, jambo ambalo haliwezi hata kidogo kutokea kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Unafikiri hapa Tanzania ingewezekana? Au unafikiri hapa TFF haifanyi ubadhirifu tena mkubwa tu? Lakini kuna kamati ambayo inaweza kumuwajibisha kiongozi wa TFF hata akiwa ni wa ngazi ya chini kabisa?
Jiulize, Rais wa TFF, Jamal Malinzi kama ataboronga au kuhusishwa na suala ambalo si sahihi, Kamati ya Maadili ya TFF inaweza kumuita na kumhoji, ikifanya hivyo itakuwa huru kufanya uamuzi sahihi? Kwangu jibu ni hapana.
Hapana kwa kuwa hata Malinzi kamati ameziteua kwa kuangalia ushikaji. Ndiyo maana unaona namna suala la Mwanasheria Damas Ndumbaro lilivyoendeshwa kibabe hadi kuchukuliwa hatua.
Kwanza, Dk Ndumbaro hakusikilizwa, halafu kwa kuwa alionekana ni mtu hatari na anayependa haki, akafungiwa harakaharaka ili watu waendeleze mambo yao. Hiyo ilikuwa ni kujizatiti zaidi.
Siku chache kabla ya hukumu ya Blatter na Platini, nilikuwa nikifikiria kuandika makala kushauri zile kamati ikiwezekana ziwe zinaundwa na kamati ya utendaji ili kuweka uhuru na haki.
![]() |
| PLATINI |
Kamati hizo zinatumika kutoa maamuzi kadhaa kwa ajili ya soka na watu wake. Suala la haki ni la msingi sana na lazima tukubali uhuru wa hizo kamati ni jambo la msingi na linapaswa kupewa kipaumbele.
Kingine ambacho nimekiona, ni kwamba Blatter na Platini wamesema wanataka kwenda kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa michezo, maarufu kama Cas, kama hawatapata haki, watakwenda Mahakama Kuu ya Uswisi kudai haki yao wakidai wameonewa.
Hiki ni kichekesho kabisa, vigogo hao ndiyo wamekuwa wakisisitiza masuala ya soka kutokwenda mahakamani kwa mujibu wa sheria na kanuni za Fifa. Vipi wao leo wanatishia kwenda mahakamani?
Fifa wanaonyesha kiasi gani walishikilia maslahi yao binafsi kama viongozi na si kwa ajili ya mpira. Ndiyo maana waliweza kujenga nguvu kubwa kwa viongozi wa soka katika nchi zetu masikini kama Tanzania na wao wakaitumia vibaya kuendelea kufanya wanavyotaka bila ya woga.
Fifa imejaa wezi na wababaishaji, ndiyo maana hata TFF wanafanya mambo yao kwa mfumo huohuo.
Msisitizo wangu, kamati zote za TFF ziwe huru, masuala ya ushikaji, kuangalia fulani ni Yanga au Simba, ananipenda au hanipendi ndiyo aingie si sahihi, ni sawa na kuibaka haki ya mchezo wa soka.
FIN.










0 COMMENTS:
Post a Comment