Staika nyota wa Stand United ya Shinyanga, Elias Maguri, kuna uwezekano
mkubwa akamwaga wino Yanga hivi karibuni na kama ikiwa hivyo, miamba hiyo ya
soka hapa nchini, itakuwa imeizidi kete TP Mazembe ya DR Congo ambayo bado
inajivutavuta katika suala la kumsajili kinara huyo wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara
Hivi karibuni, TP Mazembe ilifanya mazungumzo ya kutaka kumsajili
Maguri ili akawe mrithi wa Mbwana Samatta ambaye yupo mbioni kuondoka klabuni
hapo na kwenda kutafuta maisha nchini Ufaransa na kwingineko barani Ulaya.
Inadaiwa kuwa, TP Mazembe walifikia hatua hiyo ya kumvizia Maguri
kutokana na kuvutiwa na aina yake ya uchezaji lakini pia kiwango cha juu
alichokionyesha uwanjani msimu huu akiwa na kikosi cha Stand United pamoja na
Taifa Stars.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga, zimedai kuwa baada ya
uongozi wa timu hiyo kubaini kuwa TP Mazembe bado wanasuasua, imebidi utumie nafasi
hiyo ili uweze kumnasa nyota huyo aliyesimama peke yake kileleni kwenye chati
ya ufungaji, akiwa na mabao tisa.
“Harakati za kukiimarisha
kikosi chetu zinaendelea na hivi sasa tupo katika mazungumzo ya mwisho na
Maguri ambaye tumekuwa tukiitafuta saini yake kwa muda mrefu.
“Hata hivyo, tuliishiwa na pozi baada ya kusikia kuwa TP Mazembe
nao wametia mkono, lakini nguvu yetu imerejea upya baada ya kupata taarifa kuwa
timu hiyo ya DR Congo inaonekana kuanza kumpotezea.
“Hata hivyo mpaka sasa tumeshafikia sehemu nzuri na kuna uwezakano
siku chache zijazo kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, tutakuwa tumeshamalizana
naye,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipoulizwa Maguri kuhusiana na suala hilo, hakuonyesha kukubali
au kukataa, zaidi ya kusema: “Naomba mambo yote yanayohusu usajili wangu
tuyaache kwanza.”
Katika hatua nyingine chanzo hicho kiliongeza: “Mbali na Maguri
pia tunatarajia kumsajili beki mmoja wa pembeni kutoka Mbeya City na sasa tupo
tunaendelea kufanya naye mazungumzo ila siwezi kukutajia jina lake, tunahofia
wabaya wetu wasije kutuharibia.”
0 COMMENTS:
Post a Comment