Sare ya mabao 2-2 ya Simba dhidi ya Azam haikuwa hasara ya pointi tatu pekee kwa Wekundu hao bali iliwanyima pia wachezaji wa timu hiyo kiasi cha Sh milioni 10 walichokuwa wameahidiwa tayari.
Simba ilipata sare hiyo juzi Jumamosi kwenye mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuendelea kusalia kwenye nafasi ya nne nyuma ya Mtibwa Sugar, Yanga SC na vinara Azam FC.
Ahadi hiyo iliibuka wakati timu hizo zikiwa zimekwenda mapumziko ambapo baadhi ya viongozi walikwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kuwatia moyo wachezaji hao na ndipo mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji ya timu hiyo akatoa ahadi ya fungu hilo kama kikosi hicho kingefanikiwa kuibuka na ushindi siku hiyo.
Wakati ahadi hiyo inatolewa matokeo yalikuwa ni 1-1 na Simba iliporejea uwanjani kipindi cha pili ikajitutumua na kupata bao la pili kupitia kwa Ibrahim Ajibu kabla ya ndoto zao kuzimwa na John Bocco aliyechomoa bao hilo dakika ya 74.
“Unajua jana baada ya kuisha kipindi cha kwanza, viongozi walikuja kutuahidi fungu la milioni 10 kama tukishinda na kweli tulivyorejea uwanjani tukapata bao lakini baadaye hata haikueleweka Azam wakachomoa, wengi tumesikitika kukosa hiyo hela,” alisema mmoja wa wachezaji wa timu hiyo.







0 COMMENTS:
Post a Comment