Straika mpya Mniger, Issofou Boubacar, anayefanya majaribio Yanga SC, tayari ameshaeleza misimamo yake katika ishu nzima za pesa endapo benchi la ufundi la timu hiyo litaridhia kumpa kandarasi.
Bila kusitasita katika mazungumzo ya awali na uongozi wa timu hiyo, Mniger huyo ameweka wazi kuwa anahitaji ada ya usajili ya dola za Kimarekani 50,000 (zaidi ya Sh milioni 100) lakini pia akasema atahitaji na mshahara wa dola 5,000 (zaidi ya Sh milioni 10).
Ada hiyo ya dola 50,000 ndiyo ambayo Yanga iliitumia kumsajili straika Mzimbabwe, Donald Ngoma ambaye ni mchezaji ghali zaidi kikosini hapo.
Mpaka leo Jumatatu Mniger huyo amefikisha siku nne za majaribio lakini Kocha wa Yanga, Hans van Der Pulijm, alipoulizwa kuhusiana na ubora wa straika huyo, alisema bado anamuangalia na hawezi kusema chochote kuhusiana na kiwango chake kwa sasa.
“Bado ninamuangalia na kesho (leo Jumatatu) asubuhi, ndiyo itakuwa siku ya mwisho kufanya hivyo na baada ya hapo lolote linaweza kutokea,” alisema Pluijm.
Inaelezwa kuwa Yanga imependekeza kumpa dola 30,000 (zaidi ya Sh milioni 60) za usajili wake badala ya dola 50,000 lakini pia kwenye mshahara wakamshusha zaidi na kumuanzia wa dola 1,500 (zaidi ya Sh milioni 3) mpaka 2,000 (Sh milioni nne na ushee).
Chanzo makini kutoka ndani ya timu hiyo, kimesema kuwa mpaka sasa hakuna jibu la moja kwa moja kuhusiana na mwafaka, ingawa bado kuna mazungumzo yanaendelea mpaka hapo yatakapopatikana majibu ya benchi la ufundi kuhusiana na mchezaji huyo.
Baada ya taarifa hizo, Championi Jumatatu lilimtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha ambaye alisema: “Tumeshafanya mazungumzo ya awali na Mniger, tumepanga kumpa miaka miwili lakini kuhusu masuala mengine katika usajili yanabaki kuwa kati ya mchezaji na Yanga.
SOURCE: CHAMPIONI







0 COMMENTS:
Post a Comment