December 21, 2015

Na Saleh Ally
UHAKIKA wa kikosi cha Simba kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara unaonekana kuwa ni asilimia 30 hadi 36 tu. Hii si ile Simba ya enzi zile ambayo kila aliyekuwa akikutana nayo ni lazima ajipange.

Simba ya sasa ndiyo ile hata Ndanda FC, Toto Africans, Mbeya City, Mwadui FC wanaweza kujifananisha nayo na wakawa na uhakika mkubwa wa kushinda watakapokutana nayo.

Simba ya sasa, ndiyo ile mashabiki wake timu yao inapokuwa inacheza na timu yoyote ile ya Ligi Kuu Bara, wanakuwa na hofu kuu tena wakitamani mpira uishe haraka, angalau hata iondoke na pointi tatu.

Pointi tatu kwa Simba si kitu cha uhakika tena, kwa sasa imeingia katika kundi la zile timu ambazo kushiriki michuano ya kimataifa ni hadithi ya paka na panya. Sasa haijashiriki kwa misimu mitatu na dalili zinaonyesha haitashiriki msimu wa nne.

Misimu mitatu iliyopita, pamoja na kupoteza karibu kila sifa ya kuitwa Simba, ilibaki na sifa mbili tu. 

Kwamba rangi mbili nyekundu na nyeupe ndiyo alama yake, hii bado inaendelea kubaki. Lakini ile ya pili ya kuwa kiboko ya Yanga kila inapokutana nayo, ambayo nayo imeyeyuka baada ya kuchapwa mabao 2-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza.

Sasa sifa kubwa ambayo Simba inaweza kubaki nayo na kujisifia ni hiyo ya rangi za jezi ambazo hazitabadilika hata kama timu itakufa na ikifa basi itakufa nazo.

Umewahi kujiuliza kwa nini? Kama bado, umewahi kuwaza kipi kinawazuia Simba kukubali ambacho kiliwekwa mezani hivi karibuni na milionea Mohammed Dewji ambaye alitaka kuimiliki klabu hiyo kwa asilimia 51, zilizobaki ziwe za wanachama wengine?

Klabu kuwa na maendeleo, tajiri na yenye mafanikio inaweza kumilikiwa na wanachama na ikawa hivyo kama ilivyo kwa Barcelona na Real Madrid. Lakini tangu mwaka 1936, hilo limeshindikana kwa Simba na inakwenda inaporomoka kila kukicha.

Heshima ya nafasi ya pili au bingwa sasa inamilikiwa na Yanga na Azam FC, Simba haina chake na wanachama na viongozi waliopo wanaendelea kulilia mapenzi tu.

Kitu cha kwanza kinachoiangusha Simba ni umasikini, watu wengi wamekuwa wakikwepa kusema lakini hiyo ndiyo hali halisi.

Wanachama wengi wa Simba ni masikini, hawawezi kuchanga michango hata ya uanachama, wengi hawataki kuwa wanachama, wamebaki kuwa mashabiki.

 Hali kadhalika, hata viongozi wengi ni masikini, ndiyo maana wengi wao wameigeuza klabu hiyo ni sehemu ya kuendesha maisha yao kwa kujipatia kipato.

 Lakini hata wale walio na uwezo, nao wanapenda klabu hiyo iendelee kuwa masikini. Hawataki ijitegemee kifedha, wanajua ikiwa hivyo umaarufu wao utaisha na haitawanyenyekea na umaarufu wao utafia kapuni.

Makundi hayo ndiyo yanayoifanya Simba iendelee kuwa masikini na kamwe haitaondoka katika hali iliyonayo.

Haraka nikupe tofauti ya Simba na Azam na Yanga. Angalia hizo klabu mbili zina fedha, Yanga kutoka kwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji ingawa siku akiondoka, wanarejea katika kundi la Simba. Azam ni fedha za mmiliki wao, wana uhakika wa kuendelea kufanya vizuri.

Linapofikia suala la uendeshaji mfano kusajili wachezaji, angalia wachezaji walio Azam na wale wa Yanga, hakika hautakuwa na ubishi kwamba Simba ina wachezaji wengi wa bei rahisi na wengi viwango vyao si sahihi kuichezea timu hiyo.

Lakini inaendelea kulazimisha kwa kuwa kweli haina uwezo mkubwa wa kifedha kwa kuwa haina mtu mwenye nguvu anayeweza kuiendesha tena akiwa na sauti ya uamuzi wa mwisho. Badala yake inakwenda kwa ule mtindo wa “miluzi mingi na mbwa”.

 Simba imewahi kuwa na ndoto kama za TP Mazembe, jambo ambalo litabaki hadithi milele kama mwendo ni huu wa sasa. Kwa sasa bajeti ya TP Mazembe kwa uendeshaji kwa mwaka ni Sh bilioni 29, Yanga na Azam FC kila moja bajeti ni Sh bilioni 2.

 Bajeti ya Simba kwa mwaka ni Sh milioni 800, halafu inataka kuwa bora na tishio Afrika. Huu ni uendawazimu mwingine unaopaswa kuingizwa kwenye kitabu cha rekodi.

 Simba wamebaki wakijisifia rekodi za mwaka 1993 walipocheza fainali ya Caf wakiwa chini ya udhamini wa Azim Dewji, wakaing’oa Zamalek na kutinga makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 wakiwa chini ya udhamini wa Mohammed Dewji ‘Mo’. 

Baadaye Mo alijitoa baada ya kuona Simba haina dira akasisitiza asingekuwa tayari kuendelea kuingiza fedha zake wakati anaona hakuna maendeleo ya baadaye. Alitaka Simba ibadili aina ya uendeshwaji.


Leo amerejea, amefanya mkutano na viongozi wa Simba mara mbili, kwamba aimiliki kwa asilimia 51 na 49 zibaki kwa wanachama, inaonekana hawako tayari.

 Kuna viongozi wanafaidika kwa mengi? Labda umaarufu, wengine wanaendesha maisha yao. Hali kadhalika kuna wanachama wanafaidika mfano bajeti za waganga wa jadi na mengine mengi, hivyo wangependa timu iendelee kuwa katika mfumo wa kubabaisha kama sasa ili waendelee kuishi?
 Vipi wanamuhofia Mo Dewji? Wewe mwanachama ambaye unasema unaimiliki Simba, unajua sasa unaimiliki kwa kiasi gani na inakusaidia nini kuendelea kudorora na wewe ujisifie umiliki tu.

 Man United inamilikiwa na familia ya Glazer, Arsenal inamilikiwa na Stan Kroenke na wengine. Klabu kongwe ya Liverpool inamilikiwa na  Kampuni ya Feway Sports Group. Chelsea ni mali ya Roman Abramovic lakini timu zote hizi zina wanachama na mashabiki na wanaendelea kushangilia na maisha yanakwenda.

 Huu ndiyo wakati wa kukubali wawekezaji ili kuibadili Simba, hata kama hatakuwa Mo Dewji, badilisheni mambo na muachane na baadhi ya viongozi mlionao sasa waliokuwepo tokea miaka ya 47 na sasa wakati mwingine wanataka kila kitu ndani ya klabu kiende kwa matakwa yao, isipokuwa hivyo wanageuka kuwa akina Yuda.

 Mabadiliko Simba hayatapatikana wakati timu ikiwa haina fedha na inategemea kubadilika kutoka katika mifuko ya wachache ambao wanaendelea kuimiliki kijanja kwa faida yao, bora kuwepo na mmiliki anayetambulika ambaye atakuwa tayari kuwekeza, kujenga uwanja, kulea watoto na vijana na kuibadili kuwa klabu ya kisasa yenye timu ya kisasa. La sivyo, Simba mtaendelea kuusikia ubingwa na michuano ya kimataifa kwenye bomba miaka kenda na zaidi ijayo.





3 COMMENTS:

  1. Mo atakua amefanya jambo la busara endapo atarudi Singida na kuiomba Singida United, itakua heshima kubwa sana kwa wapiga kura wake wa zamani.

    ReplyDelete
  2. Tatizo la Simba si viongozi tu, hata WANACHAMA nao ni SHIDA!! Haiwezekani Mo anataka kuisaidia timu halafu sisi wanachama tumenyamaza kimya wakati viongozi wanalipinga jambo lenye maslahi na Klabu!Wanasimba huu ni wakati wa kuacha undondocha na kushikamana ili klabu ipige hatua na sihawa viongozi wetu ambao hawajui hata ku manage wachezaji!

    ReplyDelete
  3. Nakupongeza sana Saleh kwa kuliona hili na kulivalia njuga! Nachoweza kukushauri KALAMU yako isinyamaze mpaka hili LIMEKUWA! Usiridhike kwa kuliandika mara 1 halafu basi.... simama nalo mpaka kieleweke,.. nahuo utakuwa mchango wako wa kukumbukwa kama mwanamichezo ambaye umechangia jambo la maendeleo kwenye sekta ya michezo! Bravo comrade!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic