December 6, 2015



Na Saleh Ally
MWAKA 1838, Serikali ya kikoloni ya Uingereza ilifikia uamuzi wa kuanza kuijadili biasgara ya kilimo cha bangi nchini India. Biashara hiyo ilikuwa imenzishwa zaidi ya miaka kumi nyuma kusaidia kipato cha taifa la India.


UIngereza wasingekuwa tayari kutoa fedha Ulaya na kuzipeleka India, badala yake waliona zingeweza kutafutwa ndani ya India na kusaidia kuendesha maisha kwa watumishi waliokuwa chini ya wakoloni hao.

Lakini uamuzi wa kuanza kulijadili suala hilo ulifikiwa baada ya kuona badala ya kuwa biashara inayosafirishwa nje ya mipaka ya India, lakini ilibadilika na kuwa tatizo kwa afya ya watendaji kikazi ambao walianza kuvuta bangi, wakawa wanalala hali iliyosababisha baadaye kuundwa kwa sheria ya masuala ya kuzuia bangi.

Baada ya mjadala mrefu wa kisheria, ilionekana hivi; bangi ipigwe marufuku na Waingereza wangeshirikiana na Wahindi kuangalia biashara nyingi ambayo ingezaa maendeleo kama ilivyokuwa kwa bangi.

Hapa nyumba, YAnga na Simba ambazo ni klabu kongwe katika soka, hazilimi bangi, lakini bado hazina ndoto ya kubadili au kuboresha biashara zinazofanya katika kipindi hiki ili kuangalia njia nyingine ya maendeleo ili kujiendesha na ikiwezekana kuishi sawa na utajiri ulio sahihi kutokana na jina au mtaji walio nao.



Waingereza waliona bangi ni sehemu ya mtaji, wakautumia hadi siku walipoona madhara yanakuwa makubwa kuliko hata mafanikio kifedha.

Yanga na Simba,wala hawaoni mazoea ya maisha yao kwa mara nyingine yanaendelea kuwa madhara kwa kuwa yanazifanya klabu hizo kuendelea kudumaa na pamoja na utajiri zilizo nao, zinabaki kwua masikini na ombaomba tena tegemezi hasa, nitaeleza kwa nini.

Mara kadhaa, kumekuwa na mijadala kwamba Yanga zinakwenda katika mfumo mbaya kibishara, lazima ziwe na mfumo wa kisasa ikiwezekana ziuzwe kwa tajiri mmoja au zijiendeshe kama kampuni pekee na ndiyo zinaendelea.
Kutoka kwenye hatua moja kwenda nyingi, umekuwa ugonjwa sugu kwa Simba na Yanga. Angalia Waingereza, licha ya kuona bangi inaingiza fedha nyingi, lakini ina madhara makubwa hapo baadaye, wakabadilika.

Yanga na Simba ambao wanakufa kwa umasikini na wanatakiwa kubadilika kidogo tu waangukie kwenye utajiri, kwao imekuwa ni shida ambalo ni jambo la ajabu sana.

Hili linaonyesha moja kwa moja kwamba ni tatizo la kuwa na viongozi au wanachama wasiokuwa tayari kubadilika kwa kuwa ni waoga au wanaangalia maslahi yao pekee.

Wengi wanasema hivi, klabu za Ulaya zina utajiri mkubwa kwa kuwa zinaendeshwa chini ya matajiri waliozinunua kama vile familia ya Glazer na Manchester United, Roman Abramovich na Chelsea au Silvio Berlusconi na AC Milan.



Lakini takwimu za mwisho mwanzoni mwa mwaka huu zinaonyesha klabu mbili tajiri zaidi barani Ulaya na ikiwezekana duniani ni mali ya wanachama kama ilivyo kwa Yanga na Simba.

Klabu inayoongoza kwa utajiri barani Ulaya ni Real Madrid ya Hispania ambayo kwa mwaka imeweza kuingiza pauni bilioni 2.2 na kufuatiwa na Barcelona iliyoingiza kwa mwaka pauni bilioni 2.1 na hizi zote ni timu za wanachama.

Real Madrid na Barcelona zinamilikiwa na wanachama, lakini ukitaja 10 bora ya timu tajiri barani Ulaya, zenyewe ndiyo zinazoshika nafasi mbili za juu kwa kuingiza fedha nyingi.

Wanachama wao wanaonekana ni waelewa, wanajua nini kinachofanyika na wanakiunga mkono. Viongozi wao si wenye tamaa, wanajitambua na mambo yanafanyika kwa uwazi.

Uwazi ndiyo inakuwa silaha ya kujenga mafanikio hayo lakini Yanga na Simba, wanachama na viongozi wanatofautiana na inaonekana kila upande una maslahi yake.

Katika timu tano bora kwa utajiri Ulaya, tatu ni mali ya wanachama ingawa Bayern Munich imechanganya umiliki wa wanachama ni 75%, Adidas 8.3%, Audi na Allianz nao kila mmoja 8.3%. Lakini bado wanachama wana umiliki wa juu zaidi.

Unaweza kujiuliza Yanga na Simba hawajui wanachama ni mtaji mkubwa? Sasa vipi mbona kama wanaatamia mtaji huo utafikiri kuna siku utatotoa vifaranga? Au ubunifu wa uongozi wa klabu hizi ni mdogo? Au ni watu waoga wasio na uthubutu?

Sasa kama Ulaya ambako ndiyo soka limeendelea zaidi. Klabu tajiri zaidi ni zile mali ya wanachama, maana yake hata Yanga na Simba zinaweza kufanikiwa bado zikiwa mali ya wanachama.

Zile porojo kwamba bila ya Yanga na Simba kuachana na wanachama hazitaendelea milele, haliwezi kuwa ni kigezo kikubwa au namba moja.

Ukiangalia klabu kama Arsenal, Chelsea, Liverpool, Juventus na AC Milan ambazo zinamilikiwa na makampuni au wafanyabiashara wakubwa, zimeshindwa kuingiza faida kubwa zaidi ya Real Madrid au Barcelona kwa mwaka.

Madrid na Barcelona zimeingiza faida takribani mara nne ya Chelsea na AC Milan ambazo ni mali ya mabilionea Abramovich na Berlusconi.

Hii inaonyesha kwamba nguvu ya wanachama bado ni msingi bora kwa Yanga na Simba. Lakini unashindwa kufanya kazi kwa kuwa wahusika wakuu viongozi huenda ni waoga kuwabadili wanachama au ni waoga sana.

Kama una biashara halafu hauna mtaji wa wanunuzi ambao ni watu, nacho ninaweza kuwa kichekesho. Lakini kama una mtaji huo mkononi halafu si mbunifu wala biashara yako haina mvuto, nafikiri huo ni wendawazimu wa kipimo cha juu zaidi.

Huu ndiyo wakati ambao Simba na Yanga wanaweza kubadilisha mambo. Mafanikio ya Barcelona na Madrid kama klabu za wanachama zinaweza kuwa changamoto kwao.

Ningewashauri kuliko kuangalia kila siku timu itachezaje, basi mara moja au mbili Yanga na Simba wanaweza kufanya ziara ya masomo kimasoko ndani ya klabu za Barcelona na Madrid ili kujifunza mambo kadhaa yanayoweza kuwa muhimu kwao.

Kujifunza ni kila siku hadi mwisho ya maisha ya mwanadamu. Hivyo, Yanga na Simba waachane na uongozi na ikiwezekana wajifunze zaidi kubadilika huku wakijua kuendelea kubaki kama klabu za wanachama, hakuwezi kuzuia wao kuendelea!



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic