December 18, 2015


Na Saleh Ally
UMEWAHI kusikia baadhi ya wadau wakisema kwamba uwepo wa makocha wa kigeni katika mchezo wa soka nchini ni kazi bure, ikiwezekana bora wasiwepo kabisa ili tutumie makocha wazalendo.

Hali halisi inaonyesha wazi, kwamba Tanzania ina makocha wachache wenye uwezo mkubwa. Kikubwa changamoto bado inahitajika lakini kuwe na umakini tu katika utafutaji wa hao makocha wa kigeni.

Kama wakipatikana makocha bora kwa maana ya uwezo, basi watakuwa msaada mkubwa kwa klabu yao ambayo itaongeza ushindani na wao wataongeza changamoto katika ukuaji wa soka nchini.

Stewart John Hall raia wa Uingereza ni kocha kutoka Uingereza ambaye anainoa Azam FC. Kwa maana ya kazi na hata hesabu, huyu ni kati ya makocha ambao soka la Tanzania linawahitaji kwa kuwa wana mengi ya kutoa kama changamoto.

Hatua wanayopiga Azam FC wengi wanaweza kufikiri ni fedha pekee, lakini uwepo wa kocha kama Hall ni sehemu ya ubora unaohitajika, ushahidi ni ubora wa kikosi chake na mataji aliyobeba akiwa na Azam FC.

Katika mahojiano naye, Hall amesema kikubwa ambacho wamekuwa wakiangalia ni suala la hesabu za uhakika.

Hall anasema kamwe Azam FC haijawahi kuangalia suala la kukaa kileleni, badala yake wanaangalia suala la wastani ambalo linatokana na pointi walizojipangia pamoja na mechi wanazocheza.

SALEHJEMBE: Kila timu inapambana ipande na ikiwezekana kubaki kileleni, unafikiri unaweza kuwa bingwa bila kuwa kileleni?

Hall: Nafikiri hujanielewa, kwetu kileleni si kitu cha msingi. Badala yake kupita katika hesabu sahihi ambazo tunaziamini bila ya kujali tuko wapi. Tunaamini zikiwa sahihi, ndiyo ubingwa.

SALEHJEMBE:Unaweza kuzifafanua hesabu hizo kwa mfano?
Hall: Labda nikupe hesabu za msimu uliopita, mimi ninachoangalia ni wastani wa ushindi kwa mechi. Inakuwa hivi; kwanza tunajipangia kuwa na pointi tunazotaka kumaliza nazo ligi. Msimu uliopita zilikuwa 64, tunazigawa kwa 28 ambayo ni idadi ya mechi na wastani unakuwa 2.28. tukifanikiwa hili tayari tumebeba ubingwa.

SALEHJEMBE:Msimu huu hesabu ziko vipi?
Hall: Msimu huu tumeongeza idadi ya pointi tunazotaka, tunataka hadi mwisho wa msimu iwe 68, ikizidi itakuwa vizuri.

Championi: Kipi kilichofanya uongeze idadi ya pointi kutoka 64 hadi 68?
Hall: Tunataka pointi 68 kwa kuwa idadi ya timu mbili imeongezeka, hivyo unacheza mechi 30 badala ya 28 kama msimu uliopita. Ukichukua 68 ukagawa kwa 30, unapata wastani wa 2.3.

SALEHJEMBE:Mwendo wenu ulivyo kwa sasa mnakwenda vizuri kama mnavyotaka?
Hall: Tunakwenda vizuri, ndiyo maana hata baada ya mechi ya Simba, niliwaambia wachezaji sare bado haijatuharibia, sasa tujipange vilivyo kwa ajili ya mechi ijayo dhidi ya Majimaji.

SALEHJEMBE: Unaweza kufafanua vipi mnakwenda vizuri?
Hall: Tumecheza mechi 10, sare mbili na nane tumeshinda. Pointi 26 tulizonazo ukigawa kwa 10, unapata wastani wa 2.6 ambao ni ndani ya tunachotaka. Hakika tunalinda wastani, ukibaki juu, basi tutaendelea kubaki juu katika hesabu sahihi tunazotaka.


SALEHJEMBE:Mechi dhidi ya Simba, safu yako ya ulinzi ilionekana kuwa nyanya, wapinzani wako walipata nafasi nyingi, kama wangezitumia mngekwisha…
Hall: Uko sahihi, lakini watu hawakuona kuwa tuna majeruhi wengi katika ulinzi. Aggrey Morris, David Mwantika na Lacine Diouf. Hiyo ilichangia lakini bado timu ilicheza vizuri hasa kipindi cha pili baada ya kuingia Kipre Bolou.

SALEHJEMBE:Ulimtoa Himid Mao baada ya kuona Simba imetawala kiungo kipindi cha kwanza. Alikuwa na tatizo gani?
Hall: Tulipokwenda mapumziko, nilimueleza Himid kwamba namtoa, akakubali. Unajua Himid amechoka, ametumika mechi zote za Taifa Stars na Kilimanjaro Stars.

SALEHJEMBE: Hata Bocco na Kapombe pia walitumika, vipi hawakuchoka?
Hall: Kapombe pia hakucheza vizuri na alikuwa ana matatizo mengi katika mechi hiyo, yote ni uchovu. Angalau Bocco hakutumika sana mechi za Taifa Stars kwa kuwa walikuwa na Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta.

SALEHJEMBE: Simba walitawala sana, Kapombe na Mao wanaweza kuwa sababu pekee?
Hall: Hakuna haja ya visingizio, lakini sisi tulikaa pamoja siku tano tu baada ya Cecafa na katika michuano hiyo tulikuwa na wachezaji 14 katika timu mbalimbali za taifa.

SALEHJEMBE: Ukiangalia kikosi cha Azam FC kinaonekana ni kipana sana wakati hauna mashindano mengi sana, nini maana yake?
Hall: Wachezaji wa Azam FC ndiyo wanaoongoza kucheza mechi nyingi zaidi. Hadi sasa kama utajumlisha klabu, timu za taifa tayari wamecheza mechi 17. Lakini wa Yanga, kama mechi nyingi 14 na Simba ni 10. Angalia mbele yetu tuna michuano ya Shirikisho, Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Mapinduzi pia.

SALEHJEMBE: Hata Yanga pia hawana tofauti na nyinyi?
Hall: Sawa, huenda kila mmoja ana mipango yake lakini kwangu naona mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Azam ukijumlisha mechi za ligi, FA Cup, Mapinduzi, kimataifa na timu za taifa, anaweza kucheza mechi hadi 55. Si kidogo.

SALEHJEMBE: Kweli una kikosi kipana, lakini kwa nini umekuwa ukimbania Didier Kavumbagu kwa kumuweka nje hadi anafikia kutaka kuondoka?

Hall:…..


ITAENDELEA KESHO JUMAMOSI

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic