Yanga imejigamba inakwenda kuchukua Kombe la Mapinduzi linaloshikiliwa na watani wake Simba.
Msemaji wa Yanga, Jerry Muro amethibitisha ushiriki wa Yanga, lakini akasisitiza wanakwenda kulibeba na kurejea nalo Dar es Salaam.
“Kweli tutashiriki, lakini tunataka kuongeza makombe hivyo tunataka kulichukua Kombe la Mapinduzi na kurudi nalo Dar es Salaam.
“Tunapoamua kushiriki basi hatuwezi kufanya mzaha hata kidogo,” alisema Muro.
Lakini mabingwa watetezi Simba nao wamesthibitisha kushiriki. Maana yake wako tayari kulitetea kombe hilo.
“Kweli tumeshapokea mwaliko na tunakwenda kushiriki. Tuko tayari na tutaitumia michuano hiyo kama sehemu ya kuendelea kukijenga kikosi chetu,” alisema Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tully.
Simba ililichukua Kombe hilo ikiwa chini ya Kocha Goran Kopunovic ambaye alikabidhiwa timu akiwa Zanzibar kwa mara ya kwanza.








0 COMMENTS:
Post a Comment