January 25, 2016



DOKTA Jonas Tiboroha ameondoka Yanga, sasa atabaki kama mwanachama wa kawaida baada ya kuandika barua ya kujiuzulu.

Dk Tiboroha ambaye ni mwalimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anaondoka Yanga baada ya uongozi kumpa nafasi moja ya heshima ambayo aliitumia vizuri kuhitimisha nafasi yake hiyo ya utendaji juzi.

Uongozi wa Yanga ulimpa nafasi hiyo ya heshima, kwamba Dk Tiboroha achague kujiuzulu mwenyewe kwa hiari yake, au uchukue hatua ambayo ingekuwa ni kumfukuza kazi.

Uongozi wa Yanga ulifikia hilo, nafikiri ilikuwa ni kwa nia njema na maslahi ya klabu. Uamuzi ulifikiwa baada ya kugundua madudu ambayo yalikuwa yanamhusu mwalimu huyo wa chuo wakati wa uongozi wake.

Baada ya kuorodheshewa makosa yake yote, Dk Tiboroha alikiri na kuandika barua ya kuomba radhi akisisitiza yeye ni mwanadamu na amejifunza.

Uongozi wa Yanga pamoja na kamati ya utendaji ambayo kwa asilimia kubwa inaongozwa na watu makini, wasomi waliona haikuwa sahihi kumbakiza tena, uamuzi ukawa ni kumuacha aende kwa hiari au kumfukuza.

Suala la kwamba amekosea, hadi siku anapewa nafasi ya kuachia ngazi au atimuliwe, ni takribani wiki mbili ambazo ndani yake kulipita propaganda za ajabu ambazo mimi naona hazikuwa na mashiko na aliyeziendesha huenda hakuwa ‘fundi’ wa kufikiri, kutafakari na kuyachambua mambo kabla ya kufikiria kufanya hivyo.

Kuna habari zilianza kuenea kuwa, eti Dk Tiboroha alikuwa katika wakati mgumu, kuna watu walitaka kumng’oa madarakani kwa kuwa anazuia wizi wa fedha ndani ya klabu! 

Walioendesha kampeni hizi, hawakujua waliofikia uamuzi huo ni mabosi wa Dk Tiboroha akiwemo Mwenyekiti Yusuf Manji ambaye kamwe asingekubali mtendaji bora aondoke ndani ya klabu yake. Tena ndiye anaongoza kuzuia ubadhilifu, hivyo kama ni kweli Dk Tiboroha angekuwa anazuia, vipi aondolewe?

Kama utasema watu wanataka aondoke kwa kuwa anazuia wizi, tunajua Manji hawezi kuingia katika hilo na kama angekuwa Dk Tiboroha anaonewa, ilikuwa ni rahisi kwake kung’amua. Watu wa kamati ya utendaji hawagusi fedha, lakini ndio wanaohusika na maamuzi ya juu ya klabu. Sasa nani huyo anayezuiwa kuchukua fedha na Dk Tiboroha? Nafikiri hakuna.

Kuna baadhi ya wanachama walionyesha jazba kuu, wakidai mtendaji bora anaondolewa. Tena wakajisahau na kupitia ule mfumo wa mwaka 1947, wakati ule katibu mkuu wa Yanga alikuwa akichaguliwa na wanachama.

Wakadai asiondolewe, wakadai Dk Tiboroha ni mtendaji bora, tena wakasisitiza akiondolewa basi wanaanza kudai uchaguzi. Wakasahau kwamba Dk Tiboroha ni mwajiriwa, waliomtafuta ndiyo wanaomuondoa.

Wakasahau kuwa mwenyekiti, makamu mwenyekiti na kamati ya utendaji ndiyo watu wanaofanya kazi kwa ukaribu kabisa na Dk Tiboroha. Hivyo ubora na udhaifu wake ndio wanaoujua.

Wale waliokuwa wakimpigania, wengi wao walikuwa wamejazwa upepo kwa kupewa sababu huenda hazikuwa sahihi lakini hawakutaka kuchimbua zaidi na wakaanza kukipigania ambacho hawakuwa na uhakika nacho kama kipo au hakipo au sahihi au si sahihi.

Nafikiri wakati mzuri wa Wanayanga kutafakari kinachotokea, huenda wakatumia muda wao kuchimba zaidi kuliko kutaka kujivuruga huku wakiwa hawajui undani wa kilichotokea.

Dk Tiboroha kweli ni mtu mzuri, huenda kwa maana ya uongozi hawezi kuwa na mabaya yote. Alifanya kazi yake vizuri, alikuwa rafiki bora wa baadhi ya vyombo vya habari.


Pamoja na hivyo, lazima wajue Dk Tiboroha mwenyewe aliyakubali makosa yake na kuomba radhi. Je, wanayajua ni yapi kabla ya kuanza kukurupuka na kutumika huku wakiwa hawajui lolote? Kuweni makini ili muende na wakati.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic