NILIANZA kuzungumzia kuhusiana na nilivyochukizwa na kumuona baba mzazi wa Mbwana Samatta akiwa amekaa kwenye ngazi pale kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam akisubiri ujio wa mwanaye!
Samatta mwenyewe alilazimika kukaa chini kwenye ngazi kwa kuwa hakukuwa na maandalizi yoyote yaliyofanywa. Nikahoji kwani ile sehemu ya VIP pale uwanjani ipo kwa ajili ya akina nani hasa?
Wanaopaswa kuitumia ni watu wa aina gani? Wakirejea wasanii wameshinda tuzo za kawaida tu, wanapitishiwa kule au wazazi wao wanakuwa na nafasi ya kukaa katika sehemu nzuri wakisubiri wawasili.
Nikatoa mfano wa namna ambavyo maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walipokwenda kumpokea Kocha Mart Nooij alipokuwa anatua nchini, wakampitishia VIP. Vipi siku hiyo walishindwa kuandaa na kwenda kumpa nafasi hiyo mzee Samatta na familia yake?
Kweli alistahili kukaa chini? Najua TFF lingekuwa suala linalohusisha maslahi yao binafsi au malipo au mapato, wangesema: “Sisi ndiyo wasimamizi wakuu wa soka hapa nchini.” Lakini kwa hilo la Samatta, wao pia walikuwa wageni.
Kingine ambacho nilikiona ni kosa la kumpeleka Samatta kusherehekea kikombe alichoshinda katika ufukwe wa Wilaya ya Kinondoni, bila ya kufanya hata kidogo ziara katika sehemu yoyote ya Wilaya ya Temeke.
Nafikiri mmejisahau tu kwamba Samatta si mwanamuziki, hawezi kuwa nafasi ya kutunga wimbo na kuimba kuhusiana na mapenzi yake na Wilaya ya Temeke ambayo alikulia, akachipukia kisoka na maisha yake yote yamekuwa Temeke hata kabla ya kwenda DR Congo.
Hata kama utazungumzia aliajiriwa na Simba ambayo inatokea katika Wilaya ya Ilala, lakini mechi zote za Simba zimekuwa zikichezwa wilayani Temeke na huko ndiko Samatta aliwaonyesha TP Mazembe kwamba ana uwezo mkubwa na kama wanaweza wamchukue nao wakafanya hivyo.
Hakika katika suala la Samatta, Temeke na watu wake inahitaji heshima kubwa kuliko kawaida. Nianzie hapo kwa kusema hata ile ziara ya Samatta kuwaonyesha Watanzania katika mitaa ya Dar es Salaam haikuwa sahihi kwa kuwa ilijaa walakini mkubwa.
Mkutano wake na waandishi ulifanya wilayani Ilala ambako alianza ziara hiyo kupitia na kwenda kuimalizia Kinondoni. Hakufika Temeke ambako ndiyo makao makuu ya mafanikio yake na hata sasa, bado anaishi Temeke.
Najua Samatta haweza kujipangia ratiba, huenda aliwaheshima waandaaji lakini serikali haikuliona hilo, TFF walikubali kuendelea kuwa wageni na hawakutaka kushiriki hata kidogo. Bila kupindisha maneno hili suala halikuwa sahihi hata kidogo.
Nashangazwa na TFF kujifanya wageni sana, wakati Samatta ni mtu ambaye wameendelea kushirikiana naye mara zote katika kikosi cha timu ya taifa. Nashangazwa nao kujitenga na kujifanya kama hawahusiki sana. Je, ni kwa kuwa si suala la kuingiza fedha na badala yake ni suala la kutoa fedha?
Baadaye nikasikia, Wanatemeke kwa kushirikiana na Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo ambaye ni MwanaTMK, wameamua kuandaa sherehe ya kumpongeza mtu wao pale Dar Live, kesho Jumanne.
Sikupenda waandae wao kwa kuwa walistahili kuandaliwa na kuonyeshwa walistahili lakini kama imefikia nao wamejiandalia, basi wanastahili kujitokeza na kwenda kwa wingi.
Pamoja na yote, nafikiri TFF na hata Serikali pia walipaswa kujifunza kuhusiana na suala hilo kuwa kuna kila sababu ya kuwajali watu waliosababisha au waliokuwa na mchango na watu fulani katika jambo fulani.
Si inapofikia amepata mafanikio, basi wengine ambao walikuwa kando au hawakuwepo kabisa ndiyo wanakuwa wenyeji, wahusika wakuu na walio karibu sana huku wahusika sahihi wakitengwa. Si sahihi nasisitiza.
0 COMMENTS:
Post a Comment