January 23, 2016


Na Saleh Ally
USHINDI wa pointi sita ikiwa chini ya kocha wa muda, Jackson Mayanja umeifanya Simba kuamsha upya matumaini ya mashabiki wake ambao walikuwa wamekata tamaa.

Mwishoni kabisa chini ya Kocha Dylan Kerr, Simba ilionekana kupoteza matumaini ya kuwa timu inayopewa nafasi ya kuwania ubingwa.

Lakini sasa, kuna neno angalau na hasa kwa kuwa mambo mawili yalijitokeza: Kwanza ilionyesha soka safi katika mechi hizo mbili dhidi ya Mtibwa Sugar iliposhinda bao 1-0, halafu ikaonyesha uhai ilipoibana na kuifunga JKT Ruvu mabao 2-0.

Katika mechi mbili, Simba imekusanya pointi sita na mabao matatu huku ikiwa na safu ambayo haijafungwa hata bao moja. Huu unaweza kuwa mwaka mpya wa kuirudisha Simba sahihi katika reli.

Baada ya mechi hizo mbili za Ligi Kuu Bara, kutakuwa na siku kadhaa kabla ya Simba haijarejea tena dimbani Januari 30, itakapokuwa mwenyeji wa African Sports ya Tanga.

Mechi mbili zimeamsha matumaini, lakini ili Simba inayozidiwa pointi sita na Yanga iliyo kileleni na Azam FC katika nafasi ya pili, lazima ishinde mechi tano mfululizo ambazo ndiyo zinaweza kuiweka kwenye ramani ya zile zinazowania ubingwa, kwa uhakika.


Mechi hizo zinaanzia mechi hiyo ya wiki ijayo dhidi ya African Sports, halafu zinafuatia dhidi ya Mgambo Shooting, Simba ikiwa nyumbani tena Uwanja wa Taifa na baada ya hapo itasafiri Kanda ya Ziwa ikianzia Bukoba kuwavaa wenyeji Kagera Sugar halafu Shinyanga kuwa wageni wa Stand United kabla ya kurejea Dar es Salaam kucheza na Yanga, ikiwa ni mgeni wa watani wake.

Iwapo Simba itashinda mechi hizo tano mfululizo, kwa hesabu rahisi itakuwa na pointi 48 ambazo kama na Yanga itakuwa imeshinda mechi zake nne za mwanzo, maana yake itakuwa na 51.

Tofauti ya pointi tatu kati ya Yanga na Simba itakuwa imejengwa na upungufu wa pointi tatu ambazo Simba wamezipata kwa kuwafunga watani wao.

Kama itashindwa kuwafunga, ikashinda mechi nne, maana yake itakuwa imeshindwa kupunguza pengo la pointi sita na kuongeza pengo kuwa kubwa zaidi kwa pointi tisa, hali ambayo inaweza kuwa ndiyo jumlisho la kuiondoa Simba kwenye kugombea ubingwa kabisa.

Huenda Simba itapaswa kupambana kuhakikisha inashinda mechi hizo tano kwa sababu hiyo ya kupunguza pengo na kusogea zaidi kileleni kwa kuwa washindani wakubwa watatu kwake ni Yanga, Azam FC pia Mtibwa Sugar na Stand United.

Stand United na Mtibwa Sugar, kila upande una pointi 28. Hawako mbali na Simba haipaswi kuwadharau lakini imepata nafasi ya kupambana na Yanga na Azam FC ambazo zote zinaizidi pointi sita kila moja, hivyo ikifanya vema inaweza kujikuta inawaangusha ndege wawili kwa jiwe moja na kujiweka kileleni.


Ushindi wa mechi tano mfululizo, huenda unaweza kuamsha kwa kiasi kikubwa uchezaji bora na wa kujiamini. Pia unaweza kuinua ari ya ushindi kwa kuwa wachezaji watakuwa ni wenye kiu ya kufunga na ushindi.

Haiwezi kuwa rahisi, maana mechi hizo tano zina mchanganyiko wa mambo mengi. Mfano tatu zitakuwa za jijini Dar es Salaam, huenda Simba ikafanikiwa kucheza soka safi kutokana na ubora wa uwanja. Mbili zitakuwa mjini Bukoba na Shinyanga. Hali ya viwanja si ya kiwango kizuri sana, hivyo ni kiwango cha kujituma na kupambana na timu pinzani, pia kiwanja pinzani.

Kwa hali ilivyofikia, Simba haitakuwa tena na nafasi ya kucheza soka la visingizio kwamba ilikuwa hivi au vile. Badala yake ni kupambana kuendeleza ushindi ili kurejea relini.

Kama wakipoteza mechi moja au mbili ndani hizo tano na Yanga au Azam FC zikaendelea kushinda, suala la ubingwa litabaki kama ilivyo sasa, kwamba Simba “haimo”.

MECHI 5:
SIMBA…
Vs African Sports-Nyumbani
Vs Mgambo-Nyumbani
Vs Kagera-Ugenini
Vs Stand United-Ugenini

Vs Yanga-Ugenini

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic